Israel yapatwa na wasiwasi kwa kupanuka mahusiano ya Iran na Uturuki
Mchambuzi na mwandishi wa Israel amesema kuwa utawaka Kiizayuni umepatwa na wasiwasi mkubwa kufuatia safari ya Mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Uturuki katika fremu ya kupanua mahusiano ya pande zotei wa nchi hizo mbili.
Asaf Gibour ameeleza wasiwasi wa utawala huo kuhusiana na ziara ya Brigedia Meja Jenerali Mohammad Baqeri huko Uturuki na kuandika kuwa, safari hiyo imezusha wasiwasi mkubwa kwa Tel Aviv juu ya kupanuliwa zaidi uhusiano wa kijeshi na ulinzi kati ya Ankara na Tehran.
Mwandishi huyo wa Israel ameashiria tofauti za kimitazamo kati ya Iran na Uturuki kuhusiana na mgogoro wa miaka sita nchini Syria na kuongeza kuwa, inaonekana hivi sasa misimamo ya nchi mbili imekurubiana na kufikia kufunguliwa njia ya kuimarishwa mahusiano yao.
Naye Dore Gold, katibu mkuu wa zamani wa Wizara ya Vita ya Israel na miongoni mwa shakhsia wa karibu sana kwa Waziri Mkuu wa utawala huo wa Kizayuni Benjamin Netanyahu ameielezea safari ya Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Ankara na kupanuliwa mahusiano ya kijeshi ya Iran na nchi za eneo la Mashariki ya Kati ikiwemo Uturuki na kusema kuwa, suala hilo ni tukio lisilo jema kwa Tel Aviv. Amesema kuwa nguvu za Iran katika eneo hilo zinazidi kuongezeka siku hadi siku.
Ariel Khanna mwandishi mwingine wa Israel ameandika kuwa, Uturuki na Iran ni nguvu mbili muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati ambazo hivi karibuni zilitiliana saini mikataba ya mafuta na gesi na sasa zimegeuka na kuwa nguvu za kijeshi.
Hivi karibuni Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifanya safari nchini Uturuki na kukutana na viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo akiwemo Rais Recep Teyyip Erdogan, Waziri wa Ulinzi na mkuu wa majeshi wa taifa hilo.