Iran yalaani hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti mjini Kabul, Afghanistan
Iran imelaani vikali hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mkuu wa Afghanistan Ijumaa ambapo watu 20 waliuawa.
Katika taarifa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qassemi ametuma salamu za rambi rambi kwa serikali, taifa na familia za waathirika kufuatia jinai hiyo.
Ameongeza kuwa magaidi waliotekeleza hujuma hiyo wanalenga kuibua mivutano ya kimedhehebu na kuvuruga umoja wa taifa la Afghanistan lakini pamoja na hayo magaidi wanazidi kudhoofika siku hadi siku.
Qassemi ametoa wito kwa serikali na watu wa Afghanistan wavunje njama za maadui na waungaji mkono wao kupitia kudumisha umoja na kuimarisha usalama.
Magaidi walilipua bomu na kumimina risasi wakati Waislamu wa madehebu ya Shia walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Imam Zaman mjini Kabul na kuua shahidi watu wasiopungua 20 na kujeruhi wengine wengi. Kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS au Daesh limetangaza kuhusika na jinai hiyo.
Mwezi uliopita pia magaidi wa ISIS waliuhujumu ubalozi wa Iraq mjini Kabul na baad aya hapo wakatoa onyo kwa Waislamu wote wa madhehebu ya Shia Afghanistan kuwa maeneo yao ya ibada yatahujumiwa. Punde baada ya onyo hilo, magaidi wa ISIS walishambulia msikiti wa Mashia katika mkoa wa Herat na kuua shahidi watu 32.