Iran haitavuka mstari mwekundu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33728-iran_haitavuka_mstari_mwekundu_katika_mapatano_ya_nyuklia_ya_jcpoa
Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema nchi hii itafungamana na kuheshimu ahadi zake kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusisitiza kuwa, kamwe Tehran haitavuka mistari myekundu.
(last modified 2026-09-14T11:15:43+00:00 )
Aug 28, 2017 08:34 UTC
  • Iran haitavuka mstari mwekundu katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema nchi hii itafungamana na kuheshimu ahadi zake kwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusisitiza kuwa, kamwe Tehran haitavuka mistari myekundu.

Ameongeza kuwa, katu Iran haitawaruhusu wengine waingie katika maeneo ambayo hayakuidhinishwa katika mapatano ya nyuklia ya Julai 2015 yajulikanayo kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA).

Kwa upande wake, Ali Akbar Salehi Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran naye pia amewaambia waandishi habari kuwa, mapatano ya nyuklia ya JCPOA hayakupatikana kwa urahisi, hivyo Iran haitayaacha kwa urahisi.

Maafisa hao wa ngazi za juu nchini Iran wametoa matamshi hayo katika kujibu uchochezi wa hivi karibuni wa Marekani dhidi ya JCPOA ambao ulishika kasi wakati Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alipotembelea makao makuu ya IAEA mjini Vienna kwa amri ya Washington.

Tarehe 23 Agosti, Haley alikutana na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukia Amano na baada ya hapo alidai kuwa: "JCPOA haijatafautisha kukaguliwa maeneo ya kijeshi na yasiyo ya kijeshi nchini Iran."

Matamshi hayo kwa mara nyingine yameonyesha kuwa, Marekani ingali inajaribu kukariri madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran kupitia njia ya kuushinikiza Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Haley (kushoto) na Amano

Msimamo wa Iran kuhusu madai hayo umekuwa wazi na bayana kabisa. IAEA imeainishiwa fremu ya kazi zake na Iran imeshirikiana na wakala huo kwa mujibu wa fremu hiyo. Halikadhalika IAEA imetoa taarifa na ripoti kadhaa zinazothibitisha kuwa, Iran imeheshimu kikamilifu makubaliano ya JCPOA. Lakini nukta inayotia waswasi ni kwamba, je, ni kwa kiasi gani IAEA itaathirika kutokana na mashinikizo ya Marekani?

Katika miaka ya nyuma IAEA imeonyesha udhaifu mkubwa mbele ya mashinikizo ya Marekani. Ni wazi kuwa, iwapo IAEA mara hii itaonyesha udhaifu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, basi hadhi yake itazidi kushuka na kupata pigo. Si hayo tu bali pia pande zote zilizotia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA na Marekani yaani Umoja wa Ulaya, Russia na China pia zitapata hasara.

Nchi za Umoja wa Ulaya hivi sasa zimetia saini mikataba ya mabilioni ya dola na Iran ambapo mashirika makubwa kama Total la Ufaransa yamewekeza Iran. China na Russia pia baada ya mapatano ya nyuklia zimeimarisha uhusiano wao wa kistratijia na Iran.

Mtaalamu wa masuala ya kimataifa Hassan Beheshtipour anasema hivi kuhusu JCPOA na hatua ya Marekani ya kutototekeleza majukumu yake katika mapatano hayo: "Marekani imekiuka majukumu yake kuhusu JCPOA katika sekta mbili. Kwanza, Marekani iliahidi kuwa, itasimamisha vikwazo dhidi ya Iran lakini haijafanya hivyo. Washington inataka kuendelea kutumia vikwazo kuishinikiza Iran. Pili ni kwamba, Marekani imekiuka majukumu yake kwa kuendeleza propaganda hasi dhidi ya Iran duniani kwa lengo la kuzuia nchi mbalimbali kushirikiana na Iran."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano na Rais Rouhani

Pamoja na hayo, ukweli ni kuwa kupinga mapatano ya nyuklia ni kisingizio tu kinachotumiwa na Marekani kwani kinachopingwa na wakuu wa Washington ni Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema siku chache zilizopita katika mkutano wake na Rais Hassan Rouhani na baraza lake la mawaziri kwamba: "Inabidi katika uwanja wa udiplomasia kuwepo uharakishaji mambo, kwenda na wakati na watu kuwa macho na kusisitiza kuwa, watu walioko katika masuala ya kidiplomasia hapa nchini wana wajibu wa kuona fakhari kuwa ni wanamapinduzi na wajivunie kusimama imara katika ufanikishaji wa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu kama vile kusimama kidete kukabiliana na uistikbari, kupiga vita dhulma na kupinga mfumo wa kibeberu."