Iran yaitaka serikali ya Myanmar izuie ukiukwaji haki za Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i33744-iran_yaitaka_serikali_ya_myanmar_izuie_ukiukwaji_haki_za_waislamu_wa_rohingya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainisha wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Myanmar na imeitaka serikali ya nchi hiyo izuie ukiukwaji wa haki za Waislamu nchini humo.
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Aug 29, 2017 03:48 UTC
  • Iran yaitaka serikali ya Myanmar izuie ukiukwaji haki za Waislamu wa Rohingya

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainisha wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Myanmar na imeitaka serikali ya nchi hiyo izuie ukiukwaji wa haki za Waislamu nchini humo.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mazingira yasiyo ya kibinadamu na ukandamizaji wanaokabiliana nao Waislamu wa Myanmar na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inabainisha masikitiko na wasiwasi wake kuhusu kuendelea kukiukwa haki za Waislamu wa Myanmar jambo ambalo limepelekea wengi kuuawa na wengine kulazimika kuyakimbia makazi yao." Qassemi amesema kuheshimu haki za binadamu za kimsingi ni jambo linalosisitizwa katika sheria za kimataifa. Aidha amesema Iran inaitaka serikali ya Myanmar itumie busara na sera za wastani ili kuweza kuleta amani na maisha ya maelewano baina ya jamii zote nchini humo.

Siku ya Ijumaa jeshi la Myanmar liliwaua Waislamu zaidi ya 100 katika jimbo la Rakhine ikiwa ni wimbi jipya la mauaji dhidi ya Waislamu nchini humo. Mauaji hayo yamepelekea maelfu ya Waislamu kukimbilia Bangladesh wakihofia hujuma zaidi za jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali.

Kuna Waislamu zaidi ya milioni moja na laki tatu nchini Myanmar lakini serikali ya nchi hiyo imekataa kuwapa haki zao za kimsingi hasa uraia.

Wanajeshi wa Myanmar katika kijiji cha Waislamu

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni jamii ya wachache duniani inayodhulumiwa na kunyongeshwa zaidi. 

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Bangladesh, Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na mashambulio ya Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.