Misaada ya Iran kwa Waislamu wa Rohinghya iko tayari kutumwa
-
Ibrahim Rahimpour, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya Asia na Pasifiki
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa misaada ya Jamhuri ya Kiislamu kwa Waislamu wa Rohingya huko Myanmar iko tayari kutumwa na kwamba Tehran inafanya juhudi za kuhakikisha misaada hiyo inawafikia Waislamu hao wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kinyama.
Ibrahim Rahimpour amesema hayo usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kutaka mgogoro wa Waislamu wa Rohingya ujadiliwe wiki ijayo katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya Asia na Pasifiki ameongeza kuwa, wiki ijayo Rais Hassan Rouhani ataelekea Kazakhstan kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo kuhusiana na mgogoro huo wa Waislamu wa Myanmar.
Ijumaa ya tarehe 25 Agosti lilianza wimbi jipya la mashambulizi ya kikatili ya mabudha dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar. Tangu wakati huo hadi hivi sasa zaidi ya Waislamu elfu moja wameshauawa na karibu laki moja na 70 elfu wamekimbia makazi yao.
Mwaka 2012 jeshi la Myanmar lilianzisha mashambulizi mapya ya kikatili dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya na hadi hivi sasa serikali ya mabudha ya nchi hiyo inawanyima Waislamu hao haki zao za kimsingi kabisa kama vile uraia.