Shamkhani: Faili la kukagua vituo vya kijeshi vya Iran limeshabatilishwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i34371-shamkhani_faili_la_kukagua_vituo_vya_kijeshi_vya_iran_limeshabatilishwa
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema, mwenendo hasi na utafutaji visingizio unaofanywa na serikali ya Marekani kuhusiana na utekelezaji ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango wa Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni njama za kutaka kuyachafua makubaliano hayo ya kimataifa.
(last modified 2026-09-14T16:49:45+00:00 )
Sep 15, 2017 03:22 UTC
  • Shamkhani: Faili la kukagua vituo vya kijeshi vya Iran limeshabatilishwa

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema, mwenendo hasi na utafutaji visingizio unaofanywa na serikali ya Marekani kuhusiana na utekelezaji ahadi zake katika makubaliano ya nyuklia ya Mpango wa Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ni njama za kutaka kuyachafua makubaliano hayo ya kimataifa.

Ali Shamkhani ameyasema hayo kujibu baadhi ya matamshi yaliyotolewa na maafisa wa Washington kuhusu haki ya kukagua vituo vya kijeshi vya Iran kulingana na makubaliano ya JCPOA na kuongeza kwamba suala la kufika kwenye vituo vya kijeshi vya Iran ni faili ambalo limeshabatilishwa, na mwenendo hasi na haribifu wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusiana na makubaliano hayo ya nyuklia utapata jibu mwafaka la Iran.

Shamkhani amebainisha kuwa hakuna shughuli wala utafiti wa nyuklia unaofanywa kwenye kituo chochote cha kijeshi cha Iran na hilo limethibitishwa na ukaguzi uliofanywa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA. Kwa hivyo propaganda za vyombo vya habari vya Marekani zinafanywa kwa madhumuni ya kukidhi maslahi ya Washington na kukwepa kutekeleza ahadi na majukumu yake.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Yukia Amano (kulia) na Nikki Haley

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inachukua hatua kwa mujibu wa makubaliano yaliyoainishwa kwenye makubaliano ya JCPOA tu wala haitotekeleza chochote kile kingine nje ya makubaliano hayo.

Iran imerudia tena kutoa msimamo huo kufuatia matamshi yaliyotolewa Agosti 23 na balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukia Amano, mjini Vienna makao makuu ya wakala huo. Katika mazungumzo hayo Bi Haley alidai kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayajatafautisha kuhusu kufanyiwa ukaguzi vituo vya Iran kati ya vituo vya kijeshi na visivyo vya kijeshi.../