Bahram Qassemi: Miradi ya nyuklia ya Iran haijakengeuka azimio nambari 2231
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i35433-bahram_qassemi_miradi_ya_nyuklia_ya_iran_haijakengeuka_azimio_nambari_2231
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa siasa za Iran kuimarisha makombora yake hazijakengeuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 09, 2017 10:41 UTC
  • Bahram Qassemi: Miradi ya nyuklia ya Iran haijakengeuka azimio nambari 2231

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa siasa za Iran kuimarisha makombora yake hazijakengeuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi habari wa Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Sauti na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu leo katika kikao na waandishi habari wa ndani na nje hapa mjini Tehran kuhusu msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu katika mazungumzo yanayohusu nyuklia na makombora, Bahram Qassemi ameongeza kuwa: Hakuna mabadiliko yoyote yaliyojiri katika siasa za Iran. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa uimarishaji makombora ni sehemu ya siasa za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na  kwamba siasa hizo ni za kudumu na zitaendelezwa kwa  jadi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kusema kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitaziruhusu serikali nyingine ziingilie kivyovyote vile masuala yake ya kiulinzi. 

Kuhusu onyo lililotolewa na Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafar Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH)  kwa serikali ya Marekani kuhusu uwezekano wa kutajwa jeshi la Sepah kuwa kundi la kigaidi, Qassemi amesema anataraji kuwa katika kuendeleza makosa yake, serikali ya Marekani haitatekeleza kosa hilo la kistratejia na muhimu; hata hivyo akasema jibu la Iran litakuwa kali, la wazi na zito iwapo Marekani itatekeleza jambo hilo na kwamba itapasa kukubali matokeo ya hatua hiyo. 

Meja Jenerali Muhammad Ali Jaafari, Kamanda Mkuu wa jeshi la Sepah

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria pia kuhusu kikao kijacho cha wakuu wa Iran, Uturuki na Iraq huko Baghdad na mashauriano kuhusu kura ya maoni ya eneo la Kurdistan na kueleza kuwa, nchi hizo tatu zinaendelea kuwasiliana vizuri na kwamba tarehe ya kufanyika mazungumzo ya marais wa nchi hizo tatu itatangazwa baadaye.