Rouhani: Wamarekani wametiwa kiwewe na uwezo mkubwa wa makombora wa Iran
Rais Hassan Rouhani ameutaja kuwa ni kichekesho na dhihaka mwito wa Marekani wa kutaka kufanyika mazungumzo mapya kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuzalisha makombora kwa ajili ya kujilinda.
Siku ya Alkhamisi Bunge la Marekani lilipiga kura ya kupasisha vikwazo vipya dhidi ya Iran kutokana na mradi wake wa kuzalisha makombora ya belestiki, huku Bunge la Seneti la nchi hiyo likishinikiza kufanyika ukaguzi mkali katika vituo vyote vya kijeshi vya Iran.
Akihutubia Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) leo Jumapili, Rais Hassan Rouhani amesema: "Wametiwa kiwewe na uwezo wetu mkubwa wa silaha. Tutaendelea kuunda na kuzalisha kila aina ya silaha ambazo tunahitajia kwa ajili ya kujilinda na kulinda mipaka yetu. "
Chini ya sauti za Wabunge zilizohinikiza Bunge zisemazo "Mauti kwa Marekani", Dakta Rouhani ameongeza kuwa, Iran imeunda, inaendelea kuunda na itaunda katika siku zijazo makombora ya balestiki, huku akisisitiza kuwa miradi hiyo haikiuki makubaliano yoyote ya kimataifa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa katu haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake mkubwa wa makombora.
Kuhusu madai ya Rais Donald Trump wa Marekani kwamba Iran inaunga mkono ugaidi, Rais wa Iran amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeyapigisha magoti magenge ya kigaidi katika nchi za Syria na Iraq, jambo ambalo limezighadhabisha nchi zilizounda makundi hayo.
Akiashiria uingiliaji wa mambo na chokochoko hizo za Marekani, Rais Rouhani amesema: "Mmekuja kuvuruga amani na utulivu katika eneo. Kwa kuunda magenge ya kigaidi, mmesambaratisha usalama na utulivu katika nchi za Afghanistan na Iraq, kwa kisingizio cha eti kujaribu kupatia ufumbuzi migogori iliyopo."
Amesema tafauti na Marekani, Iran imekuwa ikiwasaidia majirani zake kuimarisha usalama, baada ya nchi hizo zenyewe kuiomba rasi Tehran iwasaidie kutatua migogoro yao.