Iran: Njama za Saudia zitaifanya itengwe na ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i36220-iran_njama_za_saudia_zitaifanya_itengwe_na_ulimwengu_wa_kiislamu
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesema uhaini na njama zinazofanywa na utawala wa kifalme wa Riyadh kila uchao katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu zitaifanya Saudi Arabia itengwe.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Nov 07, 2017 04:49 UTC
  • Iran: Njama za Saudia zitaifanya itengwe na ulimwengu wa Kiislamu

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amesema uhaini na njama zinazofanywa na utawala wa kifalme wa Riyadh kila uchao katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu zitaifanya Saudi Arabia itengwe.

Ali Akbar Velayati aliyasema hayo jana Jumatatu mjini Damascus baada ya kufanya mazungumzo na Imad Khamis, Waziri Mkuu wa Syria na kubainisha kuwa, hila hizo za Saudia hazitakuwa na tija nyingine ghairi ya kuufanya utawala wa Aal-Saud uendelee kutengwa na ulimwengu wa Kiislamu.

Dakta Velayati amefafanua kuwa: "Kila siku Saudia inabuni na kuunda njama mpya katika ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu, lakini wanatakiwa wafahamu kwamba, vitendo vyake hivyo vitasababisha Riyadh itengwe na Waislamu kote duniani na Waarabau wenzao." Mwisho wa kunukuu.

Matamshi ya Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ni radiamali kwa tuhuma zisizo na msingi zilizotolewa na muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia huko Yemen dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Imad Khamis, Waziri Mkuu wa Syria

Riyadh ilidai kuwa, Iran ndiyo iliyoipatia harakati ya Ansarullah ya Yemen kombora la balistiki la masafa marefu aina ya Borkan H2 ambalo lilivurumishwa usiku wa kuamkia Jumapili kutoka Yemen na kuulenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mfalme Khalid ulioko kwenye mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. 

Hii ni licha ya Muhammad Abdussalam, msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen kutangaza kuwa, operesheni hiyo ilifanywa na vikosi vya kujitolea vya nchi hiyo na kusisitiza kuwa mji mkuu wa Saudia sasa unafikiwa moja kwa moja na makombora ya Yemen.

Ali Akbar Velayati ameongeza kuwa, ingekuwa vyema iwapo utawala wa Riyadh ungejishughulisha zaidi na mambo ya kuwasaidia wananchi wa Saudia badala ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.