Amano: Iran imeheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika kipindi chote
Kwa mara nyingine tena Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, Yukia Amano ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA katika takriban kipindi cha miaka miwili cha mapatano hayo.
Amano aliyasema hayo jana Jumatatu mjini Washington katika kongamano la kuadhimisha miaka 60 ya wakala wa IAEA, lilililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Wasomi cha Woodrow Wilson mjini Washington.
Amesema: "Ni takriban miaka miwili tangu makubaliano ya JCPOA yaanze kutekelezwa mnamo Januari mwaka 2016, naweza kusema kuwa, Iran imetekeleza majukumu yake yote ya mapatano hayo."
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA sajari na kuashiria safari yake ya hivi karibuni hapa nchini, ameliambia kongamano hilo kuwa, Iran imechukua hatua za ziada za kuonyesha uwazi katika miradi yake ya nyuklia, na wataalamu wa wakala huo wamekuwa wakivikagua vituo vya nyuklia vya nchi hii bila wasi wasi wala vikwazo.
Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki hadi kufikia sasa umethibitisha mara nane kwamba Iran imeheshimu na kufungamana kikamilifu na makubaliano hayo ya nyuklia; huku Marekani iking'ang'ania kuwa Iran imekwenda kinyume na makubaliano hayo licha ya wakala wa IAEA kukagua mara kwa mara vituo vya nyuklia hapa nchini.