Mwanga wa kuzidi kuimarika uhusiano wa Ulaya na Iran
Is'haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza habari ya kuwekwa kwenye ajenda kuu suala la kufunguliwa ofisi ya Umoja wa Ulaya hapa mjini Tehran.
Tab'an hii si mara kwanza kwa viongozi wa Iran kuzungumzia suala la kufungua ofisi kama hiyo hapa nchini. Wakati yalipofikia kileleni mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1, maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran walizungumzia suala la kuweko mazungumzo kati yao na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na kufunguliwa ofisi kama hiyo hapa mjini Tehran.
Vile vile Is'haq Jahangiri amesema kuwa, Ulaya ina nia ya kufungua hesabu maalumu ya benki kwa ajili ya kushirikiana na Tehran. Habari hiyo nayo inaweza kuwa ni kitu kinacholeta matumaini licha ya uvunjaji mkubwa wa ahadi unaofanywa na Marekani dhidi ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Alaakullihaal, historia ya uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya inaonesha kuwa kawaida nchi za Ulaya nazo hazibakii hadi mwisho wa ahadi zao kwa Iran. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchi hizo zilikuwa zikikomba utajiri mwingi wa Iran, lakini fursa zote hizo zilifutika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambao umelikomboa taifa la Iran kutoka katika makucha ya mabeberu wa dunia. Tangu wakati huo hadi hivi sasa yaani katika kipindi chote hiki cha miongo minne, nchi za Ulaya zimekuwa zikifanya njama za kila namna za kujaribu kuivunja nguvu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mfano wa karibuni kabisa wa njama hizo za nchi za Ulaya ni kukubali kwao kushirikiana na Marekani katika kuiwekea vikwazo vya kila upande Iran. Hata hivyo njama hizo zimefeli baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Kabla ya hapo nchi za Ulaya ziliusaidia kwa hali na mali utawala wa zamani wa Iraq wa Saddam katika vita vyake vya miaka minane ulivyovianzisha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hata baada ya kumalizika vita hivyo vya miaka minane na wakati Imam Khomeini (MA) alipotoa fatwa yake mashuhuri dhidi ya Salman Rushdi kutokana na kumtukana Bwana Mtume Muhammad SAW na wake zake, kwa mara nyingine Umoja wa Ulaya ulionesha uadui wake kwa Iran kwa kuiwekea vikwazo vingine Tehran. Muda mchache baadaye na licha ya kwamba uhusiano wa Iran na Ulaya uliokuwa umeboreka kidogo kutokana na mazungumzo yaliyofanyika muongo wa 1990, Umoja wa Ulaya ulivunja tena ahadi zake na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Iran kwa madai ya uongo ya tukio la Mykonos na eti kuvunja haki za binadamu na kuunga mkono ugaidi.
Mfano mwingine wa kutokuwa na mwamana Umoja wa Ulaya katika ahadi zake kwa Iran umeonekana katika mazungumzo ya nyuklia kati ya umoja huo na Iran. Katika miaka ya mwanzoni mwa muongo wa 2000, Iran ilianzisha mazungumzo ya nyuklia kati yake na Pakistan, Ufaransa na Ujerumaini, lakini mazungumzo hayo yalikwamishwa na Marekani na Umoja wa Ulaya ukajiondoa kwenye meza ya mazungumzo kama njia ya kushirikiana na Marekani dhidi ya Iran. Hata kama nchi hizo zilirejea kwenye meza ya mazungumzo yaliyoishia kwenye mapatano ya JCPOA na kuna ishara za kila namna za kuonesha kuboreka uhusiano wa Iran na Umoja wa Ulaya kutokana na maafisa wa ngazi za juu wa umoja huo kutembelea Tehran, lakini hadi hivi sasa benki za Ulaya zimeshindwa kuiondolea vikwazo vya kifedha Iran licha ya kufikiwa mapatano ya JCPOA. Si hayo tu lakini pia wawekezaji wengi wa barani Ulaya wanashindwa kuwekeza na kuingia katika soko la Iran kwa kuhofia vikwazo vya Marekani. Labda kwa kufunguliwa ofisi ya Umoja wa Ulaya hapa mjini Tehran ikawa ni ishara nzuri ya kuboreka uhusiano wa pande mbili. Hata hivyo inabidi kuwekwe mikakati madhubuti ambayo itaweza kuzuia kupata hasara Iran kutokana na mabadiliko ya ghafla yanayoweza kufanywa na Umoja wa Ulaya ambao unaonekana ni mgumu kujipapatua kutoka katika makucha ya Marekani hasa kwa kuzingatia kuwa, inaonekana wazi kwamba serikali ya hivi sasa ya Marekani ya Donald Trump haitofurahishwa hata kidogo na kuimarika uhusiano baina ya Iran na Umoja wa Ulaya.