Ayatullah Khamenei: Vijana wenye imani wameipigisha magoti Marekani kwa kuiangamiza Daesh
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, adui amezidisha uhasama wake kwa shabaha ya kuangamiza muqawama na mapambano yaliyoanzishwa na fikra ya kimapinduzi na Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini vijana na waumini wenye istiqama wamewapigisha magoti maadui na kuthibitisha tena kivitendo kaulimbiu ya "Sisi Tunaweza" kwa kuliangamiza tezi la sarati na kitakfiri la Daesh.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo katika hadhara ya maelfu ya wapiganaji wa kujitolea wa jeshi la Basij waliokwenda kuonana naye kutoka maeneo mbalimbali ya Iran. Amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa msaada na mwongozo wa Mwenyezi Mungu na kutokana na mwamko na kuwa makini kwa Imam Khomeini na jihadi ya taifa, imeweza kuhuisha Uislamu uliokuwa ukitarajiwa na Waislamu katika kalibu ya mfumo wa kisiasa na kuweka jiwe lake la msingi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria aya za Qur'ani tukufu zinazoonesha kuwa, istiqama na kusimama kidete katika njia ya Mwenyezi Mungu kuna thawabu za Akhera na ujira wa hapa duniani yaani izza, nguvu na maendeleo na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikikabiliana na uhasama wa mabeberu, uzayuni na madola yaliyobakia nyuma kwa kipindi cha miaka 38 sasa lakini hii leo imepiga hatua kubwa za maendeleo na kuwa na nguvu kubwa mara mamia au hata maelfu zaidi ya ilivyokuwa mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu, na haya ndiyo malipo ya dunia ya kusimama kidete na kuwa na istiqama.
Ayatullah Khamenei ameitaja taathira kubwa ya kizazi cha vijana wenye imani wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati licha ya kwamba vijana hao hawakuona kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu wala Imam Khomeini na kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu kuwa ni miongoni mwa miujiza ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Amesema: "Ninyi vijana mumeweza kuipigisha magoti Marekani beberu na kuishinda".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema sababu halisi ya kuangamizwa na kushindwa tezi la saratani la Daesh ni moyo na hisi ya kujitolea na ya kibasiji na kuongeza kuwa, maadui walifanya jitihada za kutumia kundi hilo la kitakfiri na lisilo na ubinadamu kukwamisha harakati ya mapambano lakini vijana wenye imani, shauku na ari waliingia katika medani ya jihadi na kumpigisha magoti adui.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, njama kadhaa na za mara kwa mara za Marekani, uzayuni na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati zimezimwa kwa nguvu na uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na miongoni mwa mifano hai ni kuangamizwa kundi la Daesh.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kutokomezwa kundi hilo la kitakfiri na lisilo na ubinadamu kutokana na hima kubwa ya vijana na wanaume wenye imani na jitihada za watu wanaokubali muqawama na mapambano ni kazi kubwa sana na kuongeza kuwa: Baadhi ya watu katika nchi jirani hawakuamini kuwa wanaweza kuliangamiza kundi la Daesh, lakini walipoingia katika medani ya mapambano walishuhudia ushindi kwa macho yao na kuamini ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran unaosema: "Sisi Tunaweza."