Iran na Russia ni nembo ya ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i37025-iran_na_russia_ni_nembo_ya_ushirikiano_katika_vita_dhidi_ya_ugaidi
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ushirikiano baina ya nchi hii na Russia katika vita dhidi ya ugaidi ni nembo ya aina yake na mfano wa kuigwa kote duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 01, 2017 03:58 UTC
  • Iran na Russia ni nembo ya ushirikiano katika vita dhidi ya ugaidi

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ushirikiano baina ya nchi hii na Russia katika vita dhidi ya ugaidi ni nembo ya aina yake na mfano wa kuigwa kote duniani.

Es’hagh Jahangiri aliyasema hayo katika mazungumzo yake na Dmitry Medvedev, Waziri Mkuu wa Russia katika mji wa Sochi, pambizoni mwa mkutano wa Baraza la Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO.

Serikali ya Damascus iliziomba Russia na Iran kupambana na ugaidi, baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kujikuta katika hujuma za kila upande za makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao tangu mwaka 2011.

Sambamba na kuashiria mikutano ya mara kwa mara kati ya viongozi wa nchi mbili hizi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Jahangiri amesema  safari ya Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Tehran mwezi uliopita ilikuwa ya kufana, na anataraji kwamba itapelekea kuonekana matunda ya kuimarika uhusiano wa kiuchumi wa pande mbili hizo.

Ramani na bendera ya Iran na nchi wanachama wa SCO

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran amesema tangu baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, uhusiano wa kibenki wa Moscow na Tehran umeimarika mno na kuongeza kwamba, Iran inakaribisha mashirika makubwa ya mafuta ya Russia, mbali na kuwa tayari kupanua uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali kama vile sekta ya tiba na madawa.

Kwa upande wake, Dmitry Medvedev, Waziri Mkuu wa Russia ameeleza juu ya utayarifu wa nchi yake kuwekeza nchini Iran huku akitoa mwito wa kuongezwa kiwango cha uhusiano wa kibiashara wa pande mbili.

Aidha amesema fursa na njia zote ziko wazi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai SCO.