Zarif: Marekani ni mshirika wa Saudia katika uhalifu wa kivita Yemen
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa Marekani ni mshirika wa Saudi Arabia katika uhalifu na jinai za kivita zinazofanyika nchini Yemen.
Matamshi hayo yametolewa na Muhammad Javad Zarif kujibu tuhuma za serikali ya Washington iliyodai kwamba, Tehran inawapa makombora ya balestiki wapiganaji wa harakati ya Ansarullah huko Yemen.
Amesema ushahidi wowote unaooneshwa na Marekani hauwezi kufunika na kuficha uhakika kwamba, Washington ni mshirika katika jinai zinazofanyika nchini Yemen.
Akiashiria mauzo ya silaha za Marekani zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Zarif amesisitiza kuwa, Washington inawauzia silaha waitifaki wake na kuwawezesha kuua raia na kuwatesa wengine kwa njaa.
Amesema badala yake, tangu awali Iran imekuwa ikisisitiza udharura wa kusitishwa mapigano, kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Yemen na kufanyika mazungumzo nchini humo.
Matamshi hayo ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran yametolewa baada ya balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley kudai kuwa, kombora lililotumiwa na wapiganaji wa Ansarullah wa Yemen dhidi ya uwanja wa ndege wa Riyadh nchini Saudi Arabia lilitengenezwa nchini Iran.
Madai hayo ya kuchekesha yametolewa baada ya kamati ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kutangaza waziwazi kwamba, haiwezi kuthibitisha kuwepo mfungamano wowote baina ya Iran na kombora lililorushwa Riyadh na wapiganaji wa Yemen.