Iran yalaani stratijia ya usalama ya Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Stratijia mpya ya usalama wa taifa Marekani inajumuisha jitihada zilizofeli za kujaribu kuonyesha kuwa eti Iran ni tishio na hivyo inapaswa kulaaniwa."
Bahram Qassemi Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo katika taarifa Juamnne usiku kufuatia kutangazwa stratijia mpya ya usalama wa Taifa la Marekani na kuongeza kuwa, stratijia hiyo haijazingatia uhalisia wa mambo na imejaa madai ya kukaririwa pamoja na tuhuma zisizo na msingi na ndoto za baadhi ya madola katika eneo.
Jumatatu Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza stratijia yake ya usalama wa taifa ambapo alikariri tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran na Korea Kaskazini na kudai kuwa nchi hizi mbli zinalenga kuvuruga uthabiti na kutishia usalama wa Marekani na waitifake wake.
Qassemi amesema stratijia hiyo haina busara wala mlingano na ni ya upande mmoja. Amesema Marekani inatafuta sehemu ya kutupa lawama baada ya kufeli katika masuala ya kitaifa na kimataifa. Aidha amesema inaelekea kuwa watawala wa Marekani hawana irada ya kubadilisha sera zao potovu na ndio sababu Washington inatizama nchi zenye misimamo huru kama vile Iran kuwa ni tishio kwa maslahi yake.
Hali kadhalika Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema sera hiyo ya Marekani isiyo na busara bila shaka itaisukuma dunia katika ukosefu wa uthabiti na kuenea ugaidi.
China na Russia pia zimekosoa vikali stratijia hiyo ya usalama wa taifa ya Trump. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hua Chunying amelaani vikali stratijia hiyo ya Trump na kusema mtawala huyo wa Marekani bado angali ana fikra za zama za vita baridi.
Katika stratijia yake hiyo Trump ameitaja China kuwa ni nchi hasimu. Naye Dmitry Peskov msemaji wa Rais wa Russia ameitaja stratijia mpya ya Trump kuwa ni ya kibeberu. Amesema Marekani inaonekana bado inajiona kuwa mbabe peke yake katika dunia na inakataa kutambua kuwepo madola mengine yenye nguvu.