Tehran yalaani azimio la Kongresi ya Marekani dhidi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani azimio lililopasishwa na Kongresi ya Marekani ikiunga mkono machafuko ya hivi karibuni hapa nchini na kusema: Azimio hilo linaloingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine ni suala lisilokubalika.
Bahram Qassemi ametoa matamshi hayo baada ya Kongresi ya Marekani kupasisha azimio linalowaunga mkono watu waliohusika na machafuko ya siku chache zilizopita hapa nchini kwa kisingizio cha kutetea uhuru wa kujieleza. Azimio hilo limeitaka serikali ya Marekani kutumia vikwazo eti makini na vikao vya dharura vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la Haki za Binadamu la umoja huo dhidi ya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mwenendo usio wa kimantiki, usio na busara na unaopingana na sheria za kimataifa wa serikali ya Marekani wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kusema: Hatua kama kupasisha azimio, kutoa matamshi na harakati za kiusahama za Marekani dhidi ya Iran ni siasa na sera zilizofilisika na kushindwa.
Qassemi amesema maazimio kama hayo ya kukaririwa, ya kisiasa na ya kimaonyesho yanadhihirisha sura na utambulisho halisi wa Marekani wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, mambo ambayo yameshuhudiwa na taifa kubwa la Iran kwa miongo kadhaa sasa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Marekani inayodai kutetea uhuru wa taifa la Iran, imewapiga marufuku na kuwazuia Wairani kuingia katika nchi hiyo na inaendeleza uhasama na uadui dhidi ya taifa hili.
Bahram Qassemi amesema, maafisa wa serikali ya Marekani wanapaswa kujua kuwa, taifa la Iran linafuatilia kwa makini siasa na mienendo hiyo ya kindumakuwili na ikilazimu litatoa jibu mwafaka wakati mwafaka.