Spika Larijani: Wamarekani hawana uchungu na taifa la Iran
Dakta Ali Larijani, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katu Wamarekani hawawezi kuwa na uchungu na taifa la Iran kwa kutumia hadaa na ghiliba.
Dakta Larijani amesema hayo leo katika kikao cha kawaida cha Bunge ambapo sambamba na kulipongeza taifa la Iran kutokana na kushiriki kwa hamasa kubwa katika maandamano ya jana ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, mahudhurio makubwa ya wananchi katika maandamano ya Bahman 22 (11 Februari) yalikuwa ni jumbe wa wazi kwa Marekani kwamba, Marekani inapaswa kutambua kuwa, haiwezi kufikia malengo yake kwa kuingilia masuala ya ndani ya taifa hili.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza pia kwamba, mahudhurio makubwa ya jana ya wananchi wa Iran katika kilele cha maadhimisho ya miaka 39 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameonyesha kwa mara nyingine tena kwamba, wananchi wa Iran daima wako macho na hujitokeza na kuwa na mahudhurio katika medani zote nyeti.
Itakumbukwa kuwa, jana mamilioni ya wananchi wa Iran walishiriki katika maandamano ya maadhimisho ya miaka 39 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kupiga nara dhidi ya Marekani ambapo waandamanaji walisisitiza kushikamana kwao kikamilifu na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unaotawala hapa nchini.