Iran yalaani kushambuliwa ubalozi wake London, Uingereza
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya kushambuliwa ubalozi wake mjini London, na kuitaka polisi ya Uingereza kuwadhaminia usalama wanadiplomasia wa Iran nchini humo.
Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema baada ya kuvamiwa ubalozi wa Iran mjini London hapo jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa alilaani kitendo hicho, ambapo Balozi wa Uingereza mjini Tehran ameomba radhi kutokana na hujuma hiyo.
Qassemi amemnukuu mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Uingereza akisema polisi mjini London walidhibiti hali na kuwatia mbaroni watu waliouvamia ubalozi huo wa Tehran na kuishusha chini bendera ya Iran.
Kadhalika msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa wito wa kusakwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria waliopanga na kuratibu uvamizi huo dhidi ya ofisi ya kidiplomasia ya Iran mjini London.
Jana Ijumaa, vijana wa kundi moja la kidini lenye misimamo ya kufurutu ada walivamia ubalozi wa Iran mjini London na kuivunjia hesima bendera ya nchi hii. Baadhi ya duru za habari zinasema maafisa usalama wa London walifumbia macho uvamizi huo.