Bahram Qassemi: Ugaidi unapaswa kung'olewa idiolojia na mizizi yake
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine tena ameonya kuwa, ugaidi ni tihio kwa jamii ya kimataifa, na kuna haja ya kukabiliana na jinamizi hilo toka kwenye mzizi yake.
Sambamba na kulaani mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni katika nchi za Ufaransa, Afghanistan na Misri, Bahram Qassemi amesema kuna udharura kwa dunia kuungana katika jitihada za kuutokomeza ugaidi.
Amesema, "Njia pekee ya kung'oa mizizi ya ugaidi unaotishia usalama na amani ya dunia, ni kukabiliana na vyanzo vyake, ikiwemo idiolojia ya Uwahabbi, wafadhili na waungaji mkono wake."
Mripuko wa bomu hapo jana katika mji wa pwani wa Alexandria uliua watu wawili akiwemo afisa wa polisi, siku moja baada ya watu watano kuuawa baada ya mtu aliyekuwa amebeba bunduki na anayeaminika kuwa na mfungamano na kundi la Daesh kufyatua risasi ovyo na kushika watu kadhaa mateka, karibu na mji wa Carcassonne kusini mwa Ufaransa.
Jana pia watu 14 waliuawa huku wengine zaidi ya 40 wakijeruhiwa, baada ya bomu kulipuka katika lango la kuingia kwenye uwanja wa michezo katika mji wa Lashkar Gar, mkoani Helmand, kusini mwa Afghanistan.