Iran yasambaratisha kundi la kigaidi kusini mwa nchi
Vikosi vya usalama Iran vimesambaratisha kijikundi cha kigaidi kusini mashariki mwa nchi katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.
Kamanda wa Kituo cha Quds katika Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC Brigedia Jeneral Mohammad Marani amesema, “Katika oparesheni ya pamoja ya IRGC na wakaazi wa Kishia na Kisunni wa Sistan na Baluchestan, tumesambaratisha kijikundi cha kigaidi kinachofungamana na magaidi wa MKO.”
Ameongeza kuwa kinara wa kijikundi hicho cha kigaidi aliyetambuliwa kama Ahmad Sahouei, pamoja na wanachama wengine wa kijikundi hicho, waliuawa katika iparesheni iliyotekelezwa na IRGC.
Aidha amesema vikosi vya usalama vimekuwa vikifuatilia mienendo ya kijikundi hicho cha kigaidi ambacho pia kimekuwa kikitekeleza vitendo vya uhalifu kama vile mauaji na wizi na kuongeza kuwa idadi kubwa ya silaha imenaswa mikononi mwa magaidi waliouawa.
Kundi la kigaidi la MKO limetekeleza hujuma nyingi za kigiaid dhidi ya raia na maafisa wa serikali nchini Iran kwa miongo mitatu sasa. Wirani zaidi ya 17,000 wameuawa katika hujuma za kigaidi tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979 ambapo MKO wameua 12,000 kati yao.
Kundi la MKO lilikuwa limeorodheshwa na Umoja wa Ulaya kuwa kundi la kigiaid hadi mwaka 2009 lakini likaondolewa katika orodha hiyo kufuatia mashinikizo ya kisiasa. Marekani pia ililiondoa kundi hilo katika orodha ya makundi ya kigaidi Septemba 2012.