Rais Rouhani aonya kuhusu taathira hasi iwapo JCPOA itakiukwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i43594-rais_rouhani_aonya_kuhusu_taathira_hasi_iwapo_jcpoa_itakiukwa
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani dhidi ya kukiuka makubaliano ya nyuklia ya Vienna na kusisitiza kuwa, endapo Washington itajiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa kama inavyotishia, basi hatua hiyo itakuwa na matokeo mabaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2018 12:04 UTC
  • Rais Rouhani aonya kuhusu taathira hasi iwapo JCPOA itakiukwa

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya Marekani dhidi ya kukiuka makubaliano ya nyuklia ya Vienna na kusisitiza kuwa, endapo Washington itajiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa kama inavyotishia, basi hatua hiyo itakuwa na matokeo mabaya.

Rais Rouhani amesema, "Hii leo, sisi (Iran) tunatekeleza wajibu wetu wakati huu kuliko wakati mwingine wowote ule, lakini wale watakaokiuka mapatano hayo wanapaswa kuelewa kuwa, taathira hasi za hatua yao zitawaathiri wao wenyewe."

Dakta Rouhani amebainisha kuwa, taifa la Iran lipo tayari kutoa jibu mwafaka kwa pande zitakazokiuka makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA.

Rais wa Iran amesema hakuna mtu anayeweza kulitisha taifa hili na kulipigisha magoti, au kuhujumu mustakabali wenye matumaini wa nchi hii ya Kiislamu.

Rais Rouhani akihutubia umati mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran

Hapo juzi Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, chaguo kuu la Iran endapo Marekani itajitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuanzisha tena shughuli za nyuklia za taifa hili zenye malengo ya amani lakini kwa kiwango cha juu na cha kisasa zaidi.

Hayo yanajiri katika hali ambao, ripoti zote za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia (IAEA) zinaonyesha kwamba, Iran imetekeleza kikamilifu majukumu yake kuhusiana na makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa baina yake na madola sita makubwa duniani ya Marekani, Ufaransa, Uingereza, China, Russia pamoja na Ujerumani Julai mwaka 2015.