Zarif: Stratejia mpya za Trump zitafanya Marekani itengwe zaidi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema stratejia mpya zilizotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani eti dhidi ya Tehran zitaifanya Washington itengwe zaidi kimataifa.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo leo Jumapili na kubainisha kuwa, "Kwa mtazamo wangu, stratejia mpya za Marekani dhidi ya Iran zilizotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, zitapelekea kutengwa zaidi Marekani katika uga wa kimataifa."
Zarif ameongeza kuwa, mbali na Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na nchi tatu za Kiarabu kupinga makubaliano ya JCPOA, lakini jamii ya kimataifa kwa ujumla ingali inaunga mkono makubaliano hayo ya nyuklia na Iran.
Mei 21, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza kile alichokiita kuwa stratejia mpya ya Washington ya kukabiliana na Iran baada ya nchi hiyo kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ambapo alitaja masharti 12 ambayo Washington inataka eti Iran iyatekeleze.
Siku chache zilizopita, Spika wa Majilisi ya Ushauri wa Kiislamu (Bunge la Iran) alisema matamshi hayo yaliyotolewa na Pompeo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu hayana mantiki na yanaonesha kuwa waziri huyo hana ukomavu wa kisiasa.
Itakumbukwa kuwa, mnamo Mei 8, Donald Trump alitangaza uamuzi wa upande mmoja wa kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, jambo ambalo linaendelea kukosolewa na nchi nyingine za kundi la 5+1 zilizoidhinisha mapatano hayo ya kimataifa mnamo Julai mwaka 2015.