Utambulisho halisi wa Marekani kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
Kingozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, Jumatano asubuhi alikutana na Spika wa Majlisi ya Kiislamu, Bunge la Iran, wabunge na wafanyakazi wa bunge ambapo alibainisha utambulisho na malengo halisi ya Marekani katika eneo.
Kiongozi Muadhamu aliashiria kuendelea kubainika wazi zaidi dhati khabithi ya Marekani na watumiaji mabavu wengine katika uga wa kimataifa na kusema: Suala hili la kuwatenganisha maelfu ya watoto na wazazi wao nchini Marekani ni kosa kubwa sana. Mtu hawezi kustahamili kusikia vilio vya watoto hao katika televisheni. Lakini pamoja na hayo, kwa ukhabithi mkubwa walionao, Wamarekani wanawatenganisha watoto na wazazi wao wahajiri.
Ameyataja mashambulizi ya kinyama yanayofanywa na nchi kadhaa zenye silaha za kisasa kwa ajili ya kuwanyang'anya watu wanaodhulumiwa wa Yemen bandari ya al Hudaydah kuwa ni mfano mwingine wa ukhabithi wa kidhati wa madhalimu na mabeberu wa kimataifa na kusema: Maadui hao wa ubinadamu pia wanaifanyia uadui Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sababu ya kusimama kidete na kupigania uadilifu kwa taifa la Iran lakini kwa baraka zake Mwenyezi Mungu, taifa hili litaishinda Marekani na maadui wengine kutokana na kulinda umoja na mshikamano wa ndani.
Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu Marekani na watumiaji mabavu wengine katika uga wa kimataifa ni jambo linaloashiria ufahamu wa utambulisho halisi wa maadui wa ubinadamu.
Ni maadui ambao, kutokana na malengo ya kishetani na fikra za kibeberu, na kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, wanapanga njama za kubadilisha ramani ya kisiasa katika eneo. Ili kufikia malengo yao, wanatumia mbinu ambazo kidhahiri zinaonekana kuwa na uso wa kimataifa katika fremu ya makubaliano na mikataba ya kimataifa. Baadhi ya makubaliano yanatumiwa na madola ya kibeberu dunaini dhidi ya mataifa mengine.
Kuhusiana na hili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza ulazima wa kukabiliana kiuerevu na baadhi ya mikataba na mapatano ya kimataifa. Amesema: Katika hatua ya kwanza mikataba hiyo hubuniwa na kupikwa katika vikao vya madola makubwa kwa ajili ya kudhamini maslahi yao, kisha hupewa sura ya kimataifa kwa kujiunga nchi waitifaki wa madola hayo, au nchi vibaraka au zile zilizotishwa, kwa kadiri kwamba pale nchi zinazojitawala kama Iran zinapokataa mikataba hiyo hushambuliwa vikali na kwa mfano kuambiwa ni kwa nini zinakataa mkataba uliokubaliwa na nchi 150?
Matamshi ya Kiongozi Muadhamu yalikuwa na nukta muhimu sana kwa ajili ya kukabiliana na njama za madola makubwa na ya kibeberu. Hii ni kwa sababu malengo ya madola hayo ya kibeberu ni ya kina sana na yanakuja chini ya hadaa kama vile kutetea haki za binadamu, kupambana na ugaidi au kutetea demokrasia.
Ni kwa msingi huo ndio Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasisitiza kuwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ambayo imebalehe na kukomaa inapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kujitegemea katika kutunga sheria zinazohusiana na masuala kama vile ya kupambana na ugaidi na utakatishaji wa fedha chafu.
Matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wake na wabunge yalikuwa aina moja ya kukumbusha kuhusu uzoefu uliopita na pia uhalisia wa mambo hivi sasa katika sera za Marekani.
Tab'an utambulisho halisi wa Marekani umebainika wazi zaidi kutokana na nchi hiyo kukiuka na kutofungamana na mikataba muhimui ya kimataifa. Baada ya kujiondoa katika mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi wa Paris, nchi hiyo wiki hii imejiondoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na sababu kuu ya uamuzi huo ni kuwa baraza hilo limekuwa likikosoa vikali jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Kama alivyosema Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani na maadui wengine wa taifa la Iran ni watumiaji mabavu kwa maana halisi ya neno hilo na hivyo mfumo wa Kiislamu, taifa na wakuu wa Iran hawatasalimu amri mbele ya utumijaji mabavu huo.