Zarif: Iran imeishtaki Marekani ICJ kutokana na kurejeshwa vikwazo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha mashtaka dhidi ya Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kulalamikia hatua iliyo kinyume cha sheria ya Washington ya kuiwekea tena Tehran vikwazo vya upande moja.
Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter Jumatatu, Zarif amesema: "Leo Iran imewasilisha malalamiko katika mahakama ya ICJ ili kuifanya Marekani iwajibike kuhusu hatua yake ya upande moja na iliyo kinyume cha sheria ya kurejesha vikwazo."
Mnamo Mei 8, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa nchi yake imeondoka katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA, ambayo yalifikiwa baina ya Iran na madola sita makubwa duniani, yaani China, Russia, Uingereza, Ufaransa, Marekani pamoja na Ujerumani mwaka 2015. Rais wa Marekani pia alitangaza kurejesha tena vikwazo dhidi ya Iran. Hatua hiyo ya Marekani imekosolewa vikali kimataifa.
Baada ya Marekani kujiondoa JCPOA na kufuatia ombi la nchi za Ulaya la kutaka JCPOA ilindwe, Iran iliafiki kuzipa fursa mpya nchi zilizosalia katika makubaliano ya JCPOA ili ziweze kudhamini maslahi yake kivitendo wakati wa kurejea vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Mazungumzo kuhusu kadhia hiyo yangalia yanaendelea.