Meja Jenerali Suleimani: Kuanzisha vita na Iran maana yake ni kuangamia Marekani
Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameashiria bwabwaja na vitisho vya hivi karibuni vya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Iran na kusema kuwa, kuanzisha vita na taifa hili maana yake ni kuangamia suhula zote za Marekani.
Meja Jenerali Qassem Suleimani amesisitiza kuwa, endapo Marekani itaanzisha vita na Iran suhula zote za Washington zitaangamia na Iran ndio itakayoamua kumalizika kwa vita hivyo au la.
Kamanda wa Kikosi cha Quds katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ujumbe wa hivi karibuni wa Rais Trump aliouandika katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter akiitisha Iran na kueleza kuwa, si katika hadhi na heshima ya Rais wa Iran kumjibu Rais huyo wa Marekani ambaye ana lugha za vilabu vya kamari na pombe.
Meja Jenerali Qassem Suleimani amemhutubu Rais wa Marekani na kusisitiza kwamba: Je unaitisha Iran ambayo haina historia duniani ya kufanya hujuma dhidi ya nchi nyingine katika hali ambayo, unapaswa kuwauliza makamanda wa kijeshi, wanasiasa na wakuu wako wa vyombo vya usalama kwamba, katika kipindi hiki cha miongo kadhaa walifanya nini?
Qassem Suleimani ameashiria kushindwa Marekani katika kuunga mkono utawala haramu wa Israel katika vita vya siku 33 na harakati ya Hizbullah ya Lebanon na kuanza vita huko Yemen ikitoa msaada wa dola bilioni mbili ikiwa pamoja na nchi mbili za Saudi Arabia na Imarati na kusisitiza kuwa, Marekani inaitishia Iran katika hali ambayo, kwa hatua zake imeifanya Bahari Nyekundi ikose usalama na Saudia ambayo kwa miaka mingi ilikuwa nchi ya amani hii leo inawaka moto.