Kiongozi: Jeshi la Iran lijiimarishe hata kama hakuna uwezekano wa vita
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesema uwezekano wa kuanzishwa vita vya kijeshi dhidi ya Iran ni mdogo sana kwa kuzingaita hali ya hivi sasa ya kisiasa, lakini pamoja na hayo Majeshi ya Iran yanapaswa kuendelea kujiimarisha kwa mtazamo wa nguvu kazi na zana za kivita.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo Jumapili mjini Tehran wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na makamanda pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran cha Khatamul Anbiya (SAW).
Ameongeza kuwa Majeshi ya Iran yanapaswa kujiimarisha kila siku kupitia kuwa macho pamoja na usimamizi bora.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kila hatua inayochukuliwa kuimarisha uwezo wa Majeshi ya Iran ni sawa na kitendo cha ibada mbele ya Mwenyezi Mungu SWT.
Kiongozi Muadhamu akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran, ameongeza kuwa kituo hicho ni sehemu muhimu ya majeshi kwani iko katika mstari wa mbele wa kukabiliana na maadui wa Iran.
Katika kikao hicho kamanda mpya wa Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran Brigedia Jenerali Alireza Sbahifard aliwasilisha ripoti kuhusu mipango ya sasa na ya siku za usoni ya kituo hicho.
Kituo cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran cha Khatamul Anbiya (SAW) kilianzishwa Agosti 31 2008 kwa dikrii ya kihistoria ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.