Kiongozi Muadhamu: Hakuna mkwamo wala tatizo lolote nchini lisiloweza kutatuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i48728-kiongozi_muadhamu_hakuna_mkwamo_wala_tatizo_lolote_nchini_lisiloweza_kutatuliwa
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei amesisitiza kuwa hakuna mkwamo wala tatizo lolote nchini lisiloweza kutatuka.
(last modified 2026-02-05T12:50:29+00:00 )
Oct 11, 2018 16:06 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Hakuna mkwamo wala tatizo lolote nchini lisiloweza kutatuliwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei amesisitiza kuwa hakuna mkwamo wala tatizo lolote nchini lisiloweza kutatuka.

Ayatullah Khamenei ametoa sisitizo hilo katika kikao na wakuu wa mihimili mitatu ya dola cha kuchunguza masuala ya uchumi kilichofanyika jana usiku.

Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu na kupongeza hima na juhudi zinazofanywa za wakuu wa mihimili mikuu ya dola pamoja na wajumbe wa baraza kuu la uratibu wa uchumi na kueleza kwamba, jukumu kuu la baraza hilo ni kupitisha maamuzi makuu na ya utatuzi katika uga wa uchumi. Amesisitiza kuwa: Kutatua masuala ya uchumi yaliyopo nchini na kukidhi na kudhamini mahitaji ya kawaida ya wananchi kunahitaji uchapaji kazi wa kijihadi na jitihada kubwa sana.

Ayatullah Khamenei amewaagiza wajumbe wa baraza kuu la uratibu wa uchumi kuchukua maamuzi imara na ya utatuzi kuhusu masuala ya msingi na changamoto muhimu za uchumi nchini na akaongezea kwa kusema: Ili kutatua baadhi ya masuala makuu ya uchumi, kama matatizo ya mfumo wa kibenki, mzunguko wa fedha, ajira, ughali wa maisha na mchakato wa upangaji bajeti inapasa yachukuliwe maamuzi ya maana na ya kivitendo.

Rais Hassan Rouhani (katikati) akiwa na Spika wa Bunge Ali Larijani (kulia) na Mkuu wa Mahakama Ayatullah Sadiq Amoli Larijani (kushoto)

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyagawa matatizo ya kiuchumi yaliyopo katika makundi mawili ya "changamoto za ndani na za muundo wa uchumi wa nchi" na "masuala yanayotokana na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani" na akafafanua kuwa: Katika kukabiliana na kila moja kati ya mawili hayo, tumieni njia za weledi na busara za utatuzi  ambazo matokeo yake yatakuwa ni kupatikana utatuzi thabiti na endelevu wa maisha ya watu na kukata tamaa adui ya kuwa na athari silaha yake ya vikwazo.

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba, kwa azma na irada thabiti ya wananchi na viongozi na kwa kutumia uwezo usio na mbadala wa vijana na wenye vipawa wa Kiirani wenye uwezo mkubwa, sambamba na kuutumia uwezo, fursa na rasilimali adhimu za nchi, hakuna shaka yoyote kuwa matatizo ya ndani na yale ya kutwishwa yatatatuka tu.../