Waziri wa Ulinzi wa Iran aonya kuhusu kuibuka 'Hitler' wapya
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametahadharisha kuwa, iwapo dunia itaendelea kufumbia macho ukiukwaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na baadhi ya madola ya kibeberu, basi ijiandae kushuhudia watawala madikteta na makatili kama Adolf Hitler, kiongozi wa zamani wa Kinazi nchini Ujerumani.
Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema hayo katika Kongamano la Nne la Kimataifa la Tiba kwa Wanajeshi wa Nchi za Asia na Pasifiki lililofunga shughuli zake hii leo hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, Marekani inafanya ugaidi wa kiuchumi dhidi ya Iran na hata kuvuruga mchakato wa kuwapa wananchi wa taifa hili dawa na mahitaji mengine ya msingi.
Amesema taifa hili ni muhanga wa mashambulizi ya mabomu ya kemikali na vita vya kulazimishwa, na ndiposa Jamhuri ya Kiislamu hii leo inafanya juu chini kuimarisha utoaji wa tiba kwa wanajeshi ili nchi nyingine zisipitie machungu lililoyapitia taifa hili katika kipindi cha vita.
Brigedia Jenerali Hatami amebainisha kuwa, siasa za baadhi ya viongozi duniani hii leo hazitofautiani hata kidogo na zile zilizokuwa zikitekelezwa na Adolf Hitler, na kutobebeshwa dhima kumeyafanya baadhi ya madola yaendelee kufanya mauaji ya kimbari na vita kama vile vinavyoendelea hivi sasa dhidi ya wananchi wa Yemen.
Sera na misimamo ya kuchupa mipaka ya Hitler katika Vita vya Pili vya Dunia ilisababisha zaidi ya watu milioni mbili kuuawa.
Kongamano la Nne la Kimataifa la Tiba kwa Wanajeshi wa Nchi za Asia na Pasifiki lililowashirikisha wajumbe kutoka nchi 117 duniani na lililojadili umuhimu wa jamii ya madaktari ulimwenguni kulipa umuhimu suala la kuhudumia majeruhi vitani, lilianza Ijumaa hapa Tehran na kufunga shughuli zake hii leo.