Rais Rouhani: Wananchi wa Iran wamezishinda njama za Marekani kwa kusimama kidete
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i49421-rais_rouhani_wananchi_wa_iran_wamezishinda_njama_za_marekani_kwa_kusimama_kidete
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Iran wameishinda mipango na njama za Marekani kwa kusimama kwao kidete.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2018 11:11 UTC
  • Rais Rouhani: Wananchi wa Iran wamezishinda njama za Marekani kwa kusimama kidete

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, wananchi wa Iran wameishinda mipango na njama za Marekani kwa kusimama kwao kidete.

Rais Rouhani amesema hayo mwishoni mwa kikao cha pamoja cha wakuu wa Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola (yaani Serikali, Bunge na Mahakama) na kubainisha kwamba, Wamarekani walikuwa wakidhani kuwa, tarehe 5 Novemba iliyokuwa siku ya kuanza duru mpya ya vikwazo dhidi ya Iran utakuwa mwanzo wa kutimia ndoto na njozi zao zisizoagulika, lakini wananchi wa Iran wamesambaratisha ndoto zao hizo.

Kikao cha pamoja cha wakuu wa Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola (Serikali, Bunge na Idara ya Mahakama)

Rais Rouhani amesema kuwa, shabaha kuu ya Marekani ya kuiwekea Iran vikwazo visivyo halali  na kuulenga mfumo wa benki, usafirishaji mafuta na baadhi ya bidhaa za taifa hili zinazosafirishwa nje ya nchi, ni kutaka kuweka athari mbaya na hasi katika maisha ya wananchi wa Iran.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kwamba, haya matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na viongozi wa Marekani kwamba, eti Washington haina nia ya kuwashinikiza wananchi wa Iran bali wanataka kuushinikiza tu mfumo unaotawala hapa nchini, si kweli  na hata utendaji wa viongozi wa dola hilo la Magharibi umethibitisha hilo.

Akiashiria kukiri serikali ya Marekani kwamba, haiwezi kuzuia uuzwaji wa mafuta ya Iran wala kuufikisha katika kiwango cha sifuri, Rais Rouhani amesema kuwa, katika miezi ijayo Wamarekani watafahamuu vyema kwamba, walichagua njia isiyo sahihi, kwani njia hiyo itaiandalia Iran mazingira ya kuzalisha zaidi mafuta na kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na nchi jirani na rafiki.