Rouhani: Madola ya kibeberu ndiyo yaliyounda makundi ya kigaidi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i50048-rouhani_madola_ya_kibeberu_ndiyo_yaliyounda_makundi_ya_kigaidi_duniani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema madola ya kibeberu ndiyo yaliyounda na kuyafadhili kwa hali na mali makundi ya kigaidi duniani, na kwamba irada thabiti na jitihada za pamoja zinahitajika ili kulitokomeza jinamizi hilo linalotishia usalama wa dunia.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Dec 09, 2018 00:05 UTC
  • Rouhani: Madola ya kibeberu ndiyo yaliyounda makundi ya kigaidi duniani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema madola ya kibeberu ndiyo yaliyounda na kuyafadhili kwa hali na mali makundi ya kigaidi duniani, na kwamba irada thabiti na jitihada za pamoja zinahitajika ili kulitokomeza jinamizi hilo linalotishia usalama wa dunia.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumamosi katika mkutano wake na Spika wa Bunge la Pakistan ambaye yuko hapa nchini kushiriki Mkutano wa Pili wa Maspika wa Mabunge ya nchi 6 za Iran, Russia, Uturuki, China, Pakistan na Afghanistan uliomalizika jana hapa mjini Tehran.

Amesema mkutano huo uliomaliza shughuli zake hiyo jana ni wa kistratajia na wenye umuhimu mkubwa, na umejadili mikakati ya kuboresha ushirikiano wa kuimarisha usalama katika kanda hii ya Mashariki ya Kati, huku akisisitiza kuwa wale waliounda magenge ya kigaidi katika miongo kadhaa iliyopita, wamefanya uhaini mkubwa dhidi ya mataifa ya eneo hili. 

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Pili wa Maspika wa Nchi Sita mjini Tehran  

Rais wa Iran amebainisha kuwa, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ndio waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi hapa nchini Iran na kwamba Tehran na Islamabad zinapaswa kuchukua hatua madhubuti za kuzima harakati za magenge hayo katika nchi mbili hizi, sanjari na kukomesha ubeberu wa Marekani.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Pakistan, Asad Qaiser amesema Islamabad ina hamu kubwa ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Tehran katika kupambana na ugaidi na kuimarisha hali ya usalama katika eneo.

Ameongeza kuwa, hakuna upande utakaoruhusiwa kuvuruga uhusiano wa kistratajia wa Iran na Pakistan na kwamba nchi mbili hizi zinatumai kuwa zitaimarisha uhusiano wao wa kiuchumi na kibiashara pia.