Dec 14, 2018 16:01 UTC
  • Zarif: Nguvu na ushawishi wa Marekani duniani unaendelea kufifia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jitihada za Rais Donald Trump za kuzishurutisha nchi nyingine zisifanye biashara na Tehran zinaonesha bayana namna uwezo, nguvu na ushawishi wa Marekani duniani unavyofifia na kudhoofika siku baada ya nyingine.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo katika Mkutano Mkuu wa Nne wa Chama cha NEDA hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, hatua ya Washington kuzishinikiza nchi nyingine duniani ziache kufanya biashara na Tehran ni ithibati kuwa Marekani inaendelea kupoteza ushawishi wake katika anga za kimataifa.

Dakta Zarif amefafanua kuwa, "Kutokana na nafasi ya kistratajia ya Iran kijografia, historia ndefu na watu wenye izza, Jamhuri ya Kiislamu ni taifa lenye uwezo mkubwa na nafasi athirifu duniani, na hili limebainika sio tu katika kipindi cha miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu, lakini pia katika muda wa miaka elfu saba iliyopita."

Amesema ukiachilia mbali Misri, Iran ndiyo nchi yenye bajeti ndogo zaidi ya masuala ya kijeshi katika eneo. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema, "Saudi Arabia ilitumia dola bilioni 69 katika ununuzi wa silaha mwaka jana pekee, katika hali ambayo bajeti yote ya ulinzi ya Iran ilikuwa chini ya dola bilioni 16. Kwa hivyo ni nini kimetufanya tuwe na uwezo mkubwa kiasi hiki? Taifa letu ndio uti wa mgongo wa usalama wa taifa, na sisi sio chochote bila watu wetu."

Sehemu ndogo ya makombora ya Iran yaliyozalishwa hapa nchini

Mwandiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran ameashiria matamshi ya kejeli ya hivi karibuni ya Seneta wa Marekani, Lindsey Graham ambaye alisema katika mahojiano na kanali ya Fox News kwamba Saudia imebakia hai kutokana na mashinikizo ya Marekani dhidi ya Iran na kwamba iwapo Marekani itaacha kuipa himaya Riyadh, basi Wasaudia watazungumza Kifarsi ndani ya wiki moja.

Dakta Zarif amesema kuhusu kauli hiyo kuwa, "Kama Muislamu na mtu anayeishi katika eneo hili, ni fedheha kubwa kusikia matamshi ya aina hiyo kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili ni fahari kubwa katika miaka 40 iliyopita, hakuna nchi au mtu anayeweza kutoa matamshi ya namna hiyo dhidi ya Iran."

 

 

 

Tags