Shamkhani: Ubeberu wa kimataifa unataka kutoa pigo dhidi ya Iran
-
Ali Shamkhani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa nchini Iran amesema kuwa, ubeberu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani umezidisha vikwazo na mashinikizo kwa shabaha ya kutoa pigo na dhoruba dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini utashindwa na kufeli kama ilivyokuwa katika kipindi chote cha miaka 40 iliyopita.
Ali Shamkhani amesema leo kuwa, adui ameanzisha vita vya pande zote vya kiuchumi na kinafsi dhidi ya ustawi na maendeleo ya Iran na kwa msingi huo kuna udharura wa kuwa macho, kujitolea, kuwa na subira na uvumilivu, kusimama kidete na kupambana kwa ajili ya kulinda dini, nchi na taifa kama ilivyokuwa katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu.
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa amezungumzia pia hatua ya Marekani ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: Hatua hiyo ya Marekani imeonesha kuwa, nchi hiyo haisiti kukanyaga sheria na maazimio ya kimataifa hata pale inapokosa kisingizio cha kufanya hivyo.
Ali Shamkhani amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itashinda njama na mipango yote ya Rais Donald Trump wa Marekani kama ilivyofanya katika kipindi cha utawala wa rais wa kabla yake, Barack Obama.
Itakumbukwa kuwa, tarehe 8 Mei mwaka huu Marekani ilijiondoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia na kuiwekea tena vikwazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.