Marekani; sababu kuu ya ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kadiri Wamarekani watakavyoondoka haraka nchini Syria ndivyo itakavyokuwa bora kwa wananchi wa nchi hiyo.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo akijibu swali kuhusiana na suala la kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Syria na kubainisha kwamba: Wamarekani hawajamletea usalama mtu yeyote yule. Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza Disemba 2018 kwamba, wanajeshi wa nchi yake wataondoka nchini Syria. Msimamo huu unaonyesha kushindwa siasa za Wamarekani nchini Syria ambapo katika kipindi cha miaka saba iliyopita Washington haikusita hata kidogo kuwaunga mkono na kuwasaidia magaidi.
Licha ya kuwa katika hatua ya awali ilitangazwa kwamba, suala la kuondoka askari wa Marekani nchini Syria lingefanyika haraka, lakini baada ya Trump kukosolewa sana na wasiwasi ulioonyeshwa na washirika wa Marekani katika eneo la Magharibi mwa Asia, uondokaji wa wanajeshi hao sasa umetangazwa kuwa utakuwa ni wa hatua kwa hatua.
Katika fremu hii, Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amefanya safari katika eneo la Magharibi mwa Asia ili awaondolee wasiwasi washirika wa Washinghton kuhusiana na uamuzi wa Rais Trump wa kuondoa wanajeshi wa Marekani huko Syria. Viongozi wa Marekani wakitumia kisingizio cha kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio, wamekuwa wakifanya juhudi za kudhibiti mwenendo wa kuondoka wanajeshi wa nchi yao huko Syria ambao sasa umefikia katika kilele cha mivutano na hitilafu ndani ya Marekani. Viongozi wa Washington wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, kuondoka wanajeshi hao kusifasiriwe na jamii ya Marekani kwamba ni kushindwa nchi hiyo huko Syria na kupata ushindi Iran.
Katika fremu hii hii, Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani Jumatano ya juzi akiwa nchini Iraq alikutana na kufanya mazungumzo na wanajeshi wa nchi yake na viongozi wa ngazi za juu wa Baghdad na akawapa hakikisho kuhusu kuondoka wanajeshi wa Washington huko Syria sambamba na kutahadharisha kwamba, Iran bado ni tishio kwa usalama wa kanda hii. Katika safari yake mjini Baghdad, Iraq, Mike Pompeo aliiarifisha Iran kuwa tishio katika hali ambayo, sera na utendaji wa Marekani ndio chimbuko la ukosefu wa amani hii leo katika Mashariki ya Kati ikiwemo Iraq na Syria.
Ukosefu huu wa amani na usalama umefuatiwa na kuanzishwa makundi mbalimbali ya kigaidi kama Daesh, na Marekani kuyaunga mkono makundi hayo huko Iraq na Syria. Upuuzaji wa matakwa ya serikali ya Iraq katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh ni upande mwingine wa sarafu wa undumakuwili wa Marekani katika vita dhidi ya ugaidi.
Tajiriba ya kuwepo Marekani nchini Syria na Iraq haidhamini amani na usalama na hii leo malalamiko ya kuweko Wamarekani nchini Syria na Iraq yamefikia kileleni. Karim al-Muhamadawi, mjumbe wa Kamisheni ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Iraq anasema kuhusiana na jambo hili kwamba: Safari ya Mike Pompeo mjini Baghdad akitumia ndege za kijeshi, haina tofauti na tishio la mamlaka ya kitaifa ya Iraq na ni kuidhalilisha nchi hiyo ya Kiarabu.
Mbali na Iraq, hali ya sasa hivi ya Afghanistan nayo inaonyesha kuwa, kila walipotia mguu wanajeshi wa Marekani basi hakuna kilichopatikana ghairi ya ukosefu wa amani na usalama na hatimaye hilo litapelekea kushindwa siasa zake na hivyo kulazimika kuondoka katika Mashariki ya Kati.