Zarif: Kongamano lijalo la Marekani dhidi ya Iran huko Poland ni sarakasi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu amesema mkutano wa Marekani na waitifaki wake dhidi ya Iran unaotazamiwa kufanyika mwezi ujao katika mji mkuu wa Poland, Warsaw ni mwendelezo wa michezo ya kuigiza na sarakasi za Wasington.
Katika ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Dakta Mohammad Javad Zarif amesema mkutano huo hautakuwa na kitu kipya ghairi ya kuwadhalilisha watakaoshiriki.
Ameandika, "Kumbusho kwa waandaaji na washiriki wa kongamano: Walioshiriki mkutano wa mwaka jana wa Marekani dhidi ya Iran ima wamekufa, au wamedhalilika au hata kutengwa zaidi, na Iran inaendelea kuimarika wakati huu kuliko wakati wowote ule."
Dakta Zarif amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inategemea uwezo wake wa ndani katika kujidhaminia usalama na pia ustawi wa kiviwanda na wala haishughulishwi na sarakasi za maadui.
Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni radiamali kwa bwabwaja za Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye jana Ijumaa katika mahojiano na Fox News alidai kuwa, "Mkutano wa Poland wa Februari 13 na 14 utajikita katika usalama, uthabiti na amani ya eneo la Mashariki ya Kati, sambamba na kuhakikisha kuwa Iran haiendelei kuwa na ushawishi haribifu katika eneo."
Kadhalika Dakta Zarif ameikumbusha serikali ya Warsaw kuwa, Iran iliwapokea maelfu ya wakimbizi wa Poland katika Vita vya Pili vya Dunia, na hii leo nchi hiyo inataka kuwa mwenyeji wa mchezo wa kuigiza dhidi ya Iran.