Zarif: Marekani ingali inakiuka haki za Wamarekani weusi
(last modified Tue, 22 Jan 2019 08:04:26 GMT )
Jan 22, 2019 08:04 UTC
  • Zarif: Marekani ingali inakiuka haki za Wamarekani weusi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hatua ya Marekani ya kumkamata, kumadhalilisha na kumzuilia kinyume cha sheria, mwandishi wa habari wa Press TV, Marzieh Hashemi imeweka bayana tena namna nchi hiyo inavyokiuka haki za kiraia za Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter jana usiku, Mohammad Javad Zarif amesema miaka 50 baada ya kuuawa Martin Luther King, mwanaharakati mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani mwaka 1968, Marekani ingali inakiuka haki za msingi za raia wake wenye asili ya Afrika.

Dakta Zarif ameandika, "Marekani inapaswa kufafanua vipi Marzieh Hashemi, bibi na mwanahabari ni tishio kwa usafiri wa ndege, kiasi cha kukamatwa na kuzuiliwa hadi atakapomaliza kutoa ushahidi mbele ya jopo la majaji. Miaka 50 baada ya kuuawa MLK (Martin Luther King), Marekani ingali inavunja haki za kiraia za wanaume na wanawake weusi."

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Martin Luther King ambaye aliongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani enzi hizo aliuawa mwaka 1968 kwa kupigwa risasi. Baadhi ya vyanzo vya habari vilidokeza kuwa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.

Martin Luther King alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani

Familia ya Hashemi inasema mwanahabari huyo alikamatwa na maafisa wa FBI katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa St. Louis' Lambert, Januari 13 na kusafirishwa hadi Washington.

Mahakama ya Marekani imesema Marzieh Hashemi anatoa ushahidi na kusailiwa faraghani katika mji mkuu huo wa Marekani. Kwa mujibu wa Hussein, mtoto wa kiume wa Hashemi, mamake anatazamiwa kufika mbele ya jopo la majaji 23 kesho Jumatano kwa mara ya tatu, na yumkini jopo hilo likafikia uamuzi haswa kwa kuzingatia kuwa vikao viwili vilivyopita vilishindwa kuwasilisha mashitaka yoyote dhidi yake.