Jeshi la Iran lazindua 'drones' na makombora mapya
Sambamba na kukaribia maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limezindua silaha mpya za kijeshi, yakiwemo makombora ya kisasa na ndege zisizokuwa na rubani (drone).
Zana hizo mpya za kisasa zimezinduliwa na vikosi vya jeshi la Iran katika Maonyesho ya Eqtedar 40 yaliyofanyika leo katika Viwanja vya Imam Khomeini hapa mjini Tehran.
Miongoni mwa mafanikio hayo mapya ya Iran ni uzinduzi wa drone mpya ya kisasa ya Kaman-12, inayoweza kuruka kilomita 200 kwa saa kwa muda wa masaa 10 mfululizo. Ndege hiyo mpya isiyo na rubani ya Iran yenye kilo 450 na inayoweza kubeba kombora la kilo 100 ina uwezo wa kipekee wa kupaa angani kutoka katika uwanja mdogo wa ndege wenye ufupi wa hadi mita 400 pekee.
Drone iliyofanyiwa ukarabati ya Shahed-129 yenye uwezo wa kubeba mabomu erevu na inayoweza kudhibitiwa kwa kutumia teknolojia ya infrared imeimarishwa na sasa inaweza kuruka hadi umbali wa kilomita 2,000 ndani ya muda wa masaa 24.
Kombora jipya la Akhgar lenye urefu wa mita 1.7 pia limezinduliwa katika maonyesho hayo na linaweza kusafiri umbali wa kilomita 600 kwa saa. Aidha kombora la Shahin linaloweza kuzuia mitambo ya rada na mitambo ya kielektroniki ya maadui limeoneshwa kwa mara ya kwanza katika maonyesho hayo.
Maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu huanza tarehe 12 Bahman (Februari 1) kila mwaka na kuendelea kwa muda wa siku 10 maarufu kwa jina la Alfajiri Kumi.