Uropokaji na upayukaji mwingine mpya wa Trump dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i51371-uropokaji_na_upayukaji_mwingine_mpya_wa_trump_dhidi_ya_iran
Marekani, katika kipindi cha urais wa Donald Trump, imedhihirisha bila kificho kuwa imepanga na inatekeleza mpango wa kuudhoofisha na kuuangusha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2019 10:37 UTC
  • Uropokaji na upayukaji mwingine mpya wa Trump dhidi ya Iran

Marekani, katika kipindi cha urais wa Donald Trump, imedhihirisha bila kificho kuwa imepanga na inatekeleza mpango wa kuudhoofisha na kuuangusha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika kutekeleza mkakati huo, Trump alitangaza kujitoa Marekani kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran; na kwa hatua yake hiyo, Washington ikawa imeanzisha rasmi vita vya kiuchumi, ambavyo lengo lake na kuzifanya hali za maisha ya watu ziwe mbaya na kusababisha manung'uniko na machafuko ndani ya Iran. Lakini kwa upande wa kieneo pia, kwa kutumia hoja ya kutekeleza hati ya mwaka 2017 ya stratejia ya usalama wa taifa wa Marekani, serikali ya Trump imechukua hatua kubwa kwa madhumuni ya kuanzisha muungano wa kieneo, lengo likiwa ni kuidhibiti na kuibana Iran ili ibadilishe sera na hatua inazochukua katika eneo hili la Mashariki ya Kati.

Trump akihutubia Kongresi ya Marekani

Katika hotuba ya kila mwaka aliyotoa jana Jumanne mbele ya wabunge wa Kongresi ya Marekani, kwa mara nyingine, Trump alirudia tena madai na tuhuma zake za hapo kabla dhidi ya Iran. Rais wa Marekani aliitaja Iran kuwa ni mfadhili na muungaji mkono mkubwa zaidi wa ugaidi. Lakini inavyoonekana Trump amesahau kwamba, wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa Marekani, yeye mwenyewe alitamka hadharani kuwa, serikali ya mtangulizi wake Barack Obama ndiyo iliyohusika na uundaji wa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS).

Trump aidha ametetea kujitoa Marekani katika makubalino ya nyuklia ya JCPOA. Kwa madai yake, alichukua hatua hiyo kutokana na Iran kuendeleza harakati za kutaka kumiliki silaha za nyuklia. Lakini ajabu ni kuwa, hakuna hata moja kati ya nchi zinazounda kundi la 5+1 wala Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ambao ndio wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa JCPOA iliyounga mkono madai hayo ya uongo ya Trump kuhusu shughuli za nyuklia za Iran, na badala yake zimethibitisha kwamba, Tehran imeyatekeleza kikamilifu makubaliano hayo.

Katika hotuba yake hiyo mbele ya wabunge wa Marekani, Trump alikiri kwa kusema: Msimu uliopita wa Mapukutiko tuliwawekea (Iran) vikwazo vikali zaidi kuwahi kuiwekea nchi yoyote ile hadi sasa. Rais huyo wa Marekani, mbali na kuyakosoa vikali mara kadhaa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, amekuwa akisisitiza pia kwamba, kwa kutumia vikwazo, Washington itailazimisha Tehran iyakubali matakwa yake. Lakini ukweli ni kwamba, sera ya vikwazo ya Marekani dhidi ya Iran imeshindwa na kufeli kikamilifu. Na hasa kwa kuzingatia kwamba, nchi zinazounda kundi la 4+1, yaani Russia, China pamoja na Troika ya Ulaya inayojumuisha Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinapinga hatua ya kuiwekea Iran vikwazo vya kidhalimu.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Trump ameituhumu Iran kuwa ina chuki na Mayahudi (Antisemitism). Akilizungumzia suala hilo, rais wa Marekani amesema: Sisi hatutaacha katu kuuandama utawala unaotoa kauli mbiu ya Mauti kwa Marekani na kutishia kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Mayahudi. Trump amezusha tuhuma hizo ilhali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshasisitiza mara kadha wa kadha kuwa, inapasa itafautishwe kati ya Wayahudi na Wazayuni. Inachopinga Iran ni utawala wa Kizayuni wa Israel, ambao kwa miongo kadhaa sasa umenyakua na kuighusubu ardhi ya Palestina; na kwa uungaji mkono wa wazi wa Magharibi na hasa Marekani, sera yake kuu ni kuwakandamiza na kuwadhulumu bila kificho Wapalestina, sambamba na kuanzisha uchokozi wa kuzivamia nchi jirani.

Mayahudi wenyewe wakiandamana kupinga utawala wa Kizayuni wa Israel

Hivi sasa Trump anajulikana rasmi kuwa ndiye muungaji mkono mkubwa zaidi wa Israel, ambapo katika kulithibitisha hilo, mwezi Desemba mwaka 2017 aliitambua rasmi Baitul Muqaddas (Jerusalem) kuwa mji mkuu wa utawala huo wa Kizayuni na kuamuru ubalozi wa Marekani uliokuweko Tel Aviv uhamishiwe katika mji huo. Lakini mbali na hayo, Trump amekuwa akiunga mkono kikamilifu pia misimamo ya kiuadui ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu dhidi ya Iran, na kutilia mkazo kuanzishwa muungano wa kikanda dhidi ya Tehran kupitia mhimili wa pande tatu za Marekani, utawala wa Kizayuni na utawala wa Aal Saud.

Kwa mujbu wa Sayyid Ahmad Hosseini, mchambuzi wa masuala ya kimataifa: Kuyavuruga makubaliano ya JCPOA, kurejesha vikwazo, kutoa mashinikizo kwa lengo la kuzifunga njia za mabadilishano ya kifedha, kufanya chokochoko za kuisukuma Iran ili ichukue hatua zitakazoigharimu pakubwa, kuwawekea mbinyo wananchi ili wasimame dhidi ya utawala na kuendeleza vitisho na lugha ya vita ni miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali ya sasa ya Marekani ili Iran ionekane tishio na hatari kwa eneo na ulimwengu mzima.

Lakini licha ya madai ya Trump, ambaye amejaribu kuonyesha kuwa Iran imetengwa na iko kwenye mashinikizo, hivi sasa ulimwengu umeshabainikiwa vyema kwamba mtazamo wa kupindua utawala ilionao serikali ya Trump kuhusiana na Iran, umetokana na chuki na uadui wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa sababu ya ungangari na kusimama kwake kidete kukabiliana na sera za kibeberu za Washington na uingiliaji wake katika masuala ya Iran na eneo. Ukweli ni kwamba, sera za Marekani za kutaka kuuangusha Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hazitakuwa na matokeo mengine zaidi ya kuzidisha mshikamano wa kitaifa wa Wairani na kuimarisha moyo wao wa kupambana na ubeberu na uistikbari.../