Rouhani: Iran inakaribisha suala la kuimarisha uhusiano na Japan
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54088-rouhani_iran_inakaribisha_suala_la_kuimarisha_uhusiano_na_japan
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa hamu iliyodhihirishwa na Japan ya kutaka kuwekeza katika maeneo ya kusini mwa Iran inadhamini suala la kustawisha uhusiano kati ya nchi mbili.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jun 12, 2019 23:38 UTC
  • Rouhani: Iran inakaribisha suala la kuimarisha uhusiano na Japan

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa hamu iliyodhihirishwa na Japan ya kutaka kuwekeza katika maeneo ya kusini mwa Iran inadhamini suala la kustawisha uhusiano kati ya nchi mbili.

Rais Hassan Rouhani aliyasema hayo jana usiku katika kikao na waandishi wa habari hapa Tehran akiwa pamoja na mgeni wake Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na kuongeza kuwa uhusiano wa Iran na Japan ni wa kihistoria na mwaka huu nchi mbili zinaadhimisha mwaka wa 90 wa uhusiano huo.   

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa serikali ya Japan na Waziri Mkuu wa nchi hiyo wamedhamiria kukuza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, kikandea na kimataifa na Iran inaunga mkono suala hilo. Amesema mbali na kujadili masuala ya pande mbili, katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Japan wamezungumzia pia suala la usalama na kuondoa hali ya mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati. 

Rais wa Iran akiwa katika amzungumzo Tehran na Waziri Mkuu wa Japan
 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa Waziri Mkuu wa Japan ana matarajio makubwa kuhusu masuala ya kieneo na kwamba Iran inafurahishwa na hatua ya Japan ya kuendelea kuyaunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutambua umuhimu wa makubaliano hayo kwa ajili ya eneo hili na ulimwengu kwa ujumla.

Katika kikao hicho na waandishi wa habari pamoja na Rais wa Iran, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema kuwa ushirikiano wa nchi yake na Iran zikiwa nchi kongwe, za kihistoria na nchi kubwa zenye tamaduni umekuwa ukiendelezwa kupitia mahusiano ya wananchi wa nchi mbili hizo.

Abe amesisitiza kuwa kupunguza hali ya mivutano katika Mashariki ya Kati ni miongoni mwa matarajio ya nchi yake na kueleza kuwa, amefanya ziara nchini Iran kutokana na kulipa umuhimu suala hilo. Shinzo Abe amesema Uislamu ni dini ya amani na uvumilivu na kueleza kuwa, siku zote amekuwa akiathiriwa na  mafundisho ya kimaanawi ya Uislamu na kwamba anampa heshima kubwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambaye anasisitiza kuwa silaha za maangamizi ya umati zikiwemo silaha za nyuklia ni haramu kwa mujibu wa dini ya Kiislamu.