Rouhani: Bodi ya IAEA imepuuza njama za Marekani dhidi ya Iran
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya kuendelea kutengwa Marekani katika uga wa kimataifa na kusema kuwa, mbali na nchi moja au mbili, nchi zote wanachama wa Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) katika kikao chao cha hivi karibuni zilipuuza njama za Marekani dhidi ya Iran.
Rais Rouhani amesema hayo leo katika mji wa Shirvan, mkoani Khorasan Kaskazini huko kaskazini mashariki mwa nchi ambapo ameeleza bayana kuwa, licha ya Marekani kuitisha kikao maalumu cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) hivi karibuni, lakini njama zake dhidi ya Iran kwa kutumia bodi hiyo zilifeli.
Dakta Rouhani amefafanua kuwa, "Kupuuzwa Marekani katika kikao hicho cha IAEA ambacho kiliitishwa na Marekani yenyewe ni ushindi mkubwa kwa Iran na pigo kwa Wamarekani."
Amesema licha ya changamoto, mashinikizo na vikwazo, lakini taifa hili limeweza kuruka viunzi vingi kiasi cha kufanikiwa kupunguza kiwango cha deni lake la nje kwa asilimia 25.
Rais wa Iran anatazamiwa kuzindua miradi 132 hususan ya miundombinu katika mkoa huo wa Khorasan Kaskazini huko kaskazini mashariki mwa nchi.
Kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) kilifanyika siku chache zilziopita huko Vienna Austria makao makuu ya wakala wa IAEA kufuatia ombi la Marekani.
Marekani ilitaka kufanyika kikao hicho cha dharura ili kuchunguza hatua za karibuni za Iran za kupunguza utekelezaji wa ahadi zake kuhusiana na makubaliano ya JCPOA, lakini kikao hicho kilimalizika bila ya matunda yoyote kwa Marekani.