Usalama wa Ghuba ya Uajemi utadhaminiwa kwa ushirikiano wa majirani
Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejadiliana, kupitia mazungumzo ya simu, na Mawaziri wenzake wa Ulinzi wa Qatar, Oman na Kuwait kuhusu umuhimu wa kudhaminiwa usalama wa Ghuba ya Uajemi kupitia ushirikiano wa pamoja.
Katika mazungumzo hayo Brigedia Jenerali, Amir Hatami amesema: Usalama wa eneo utadhaminiwa tu na nchi za eneo hili na kuwa kuwepo kwa majeshi ya kigeni katika eneo hakuna matokeo mengine isipokuwa kuibua ghasia na machafuko.
Akiashiria kisingizio kinachotumiwa na Marekani kwa ajili ya kubuni muungano eti wa kudhamini usalama wa baharini katika Ghuba ya Uajemi na pia suala la kuwepo Wazayuni katika muungano huo, Brigedia Jenerali Hatami ametahadharisha juu ya jambo hilo na kusisitiza kwamba muungano wa kijeshi ambao unataka kubuniwa na Marekani kwa kisingizio cha kulinda usalama wa meli za mafuta katika Ghuba ya Uajemi hautakuwa na natija nyingine ghairi ya kuongeza mivutano katika eneo.
Baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusimamisha meli moja ya ulanguzi wa mafuta na pia meli nyingine ya mafuta ya Uingereza zilizokuwa zimekiuka sheria za kimataifa, ikiwa katika kutekeleza majukumu yake ya kulinda usalama wa baharini katika maji ya Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, Marekani imekuwa ikitumia kisingizio hicho kujaribu kubuni muungano wa kijeshi wa baharini kwa madai ya kulinda usalama wa eneo hili.
Iran ikiwa ni nchi inayowajibika kimataifa, ina nafasi muhimu katika kulinda uwiano wa kieneo na kwa kulinda usalama wa baharini, imekuwa na wajibu muhimu wa kudhamini usafirishaji salama wa nishati kuelekea masoko ya dunia kupitia Lango Bahari la Hormuz.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba usalama ni suala la ushirikiano wa pamoja wa nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi na kwamba uwepo wa wageni katika eneo hili la kijografia bila shaka hausaidii lolote latika kudhamini usalama na uthabiti wa eneo hili.
Iran daima imekuwa ikiuchukulia ushirikiano na majirani kuwa msingi muhimu katika siasa zake za kigeni na kutokana na umuhimu wa kistratejia wa Ghuba ya Ujemi, imekuwa ikiupa umuhimu mkubwa msingi huo kwa lengo la kudhamini usalama wa eneo na hasa wa maji ya Ghuba ya Ujemi kwa madhumuni ya kudhaminiwa uthabiti wa soko la mafuta duniani.
Daima imekuwa ikitaka kufanyike mazungumzo baina yake na majirani zake katika Ghuba ya Ujemi na ni kwa msingi huo ndipo waziri wake wa mambo ya nje akatoa pendekezo la kutiwa saini mapatano ya nchi jirani kutoshambuliana.
Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni aliashiria umuhimu wa suala hilo na kusema kwamba ni jambo la dharura kuasisiwa jumuiya ya kieneo ya mazungumo na kutiwa saini mkataba wa nchi jirani kutoshambuliana.
Ubunifu na diplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi imesimama katika msingi wa kunufaika na uwezo wa ndani ya nchi na kieneo kwa lengo la kusimamia masuala ya eneo na bila shaka uingiliaji wa wageni katika jambo hilo hautakuwa na mslahi yoyote kwa nchi za eneo hili.
Kwa kutegemea suhula na uwezo wake wa ndani ya nchi, Iran imefanikiwa kudhamini usalama wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz jambo linalothibitisha wazi nafasi muhimu ya Jamhuri ya Kiislamu katika kudhamini uslama na utulivu wa eneo.
Kuhusiana na suala hilo, Khalid bin Muhammad bin Abdallah al-Atiyya, Waziri wa Ulinzi wa Qatar amezungumza na Waziri wa Ulinzi wa Iran na kumwambia: Usalama wa Ghuba ya Uajemi unapasa kudhaminiwa na nchi za pande zote mbili za ghuba hii na bila shaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi muhimu sana katika kulinda usalama wa Ghuba ya Uajemi.
Naye Sheikh Nassir Swabah al-Ahmad as-Swabah, Waziri wa Ulinzi wa Kuwait anaamini kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu na athirifu mno katika kulinda usalama na uthabiti wa Ghuba ya Uajemi.
Kwa kutilia maanani suhula na uwezo wa eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi, ushirikiano wa pamoja wa nchi za eneo hili bila shaka utaweza kudhamini na kukidhi mahitaji yao na hivyo kuondoa tabia ya kuzitegemea nchi za kigeni kudhamini mahitaji hayo. Kwa msingi huo, usalama na uthabiti wa kudumu utakuwa umeandaliwa katika eneo la kistratejia la Ghuba ya Uajemi.