Iran: Jaribio la kombora la Marekani litazusha mashindano ya silaha duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55580-iran_jaribio_la_kombora_la_marekani_litazusha_mashindano_ya_silaha_duniani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea wasiwasi wake kutokana na Marekani kufanyia majaribio kombora lake la masafa ya wastani na kusema kuwa, jaribio hilo litazusha ushindani wa silaha ulimwenguni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 24, 2019 22:05 UTC
  • Iran: Jaribio la kombora la Marekani litazusha mashindano ya silaha duniani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelezea wasiwasi wake kutokana na Marekani kufanyia majaribio kombora lake la masafa ya wastani na kusema kuwa, jaribio hilo litazusha ushindani wa silaha ulimwenguni.

Sayyid Abbas Mousavi vile vile amelaani kitendo cha Marekani cha kung'ang'ania siasa zake zake za kujitoa kwenye mikataba ya kimataifa na kudhoofisha sheria na kanuni za kimataifa na kuongeza kuwa, hatua ya Marekani ya kulifanyia majaribio kombora lake hilo la masafa ya kati mbali na kushadidisha ukosefu wa utulivu na kuhatarisha amani na usalama wa kimataifa, itazisababishia nchi nyingine za dunia, hasara kubwa ya kiuchumi.

Hatua ya Marekani ya kujitoa katika mkataba wa silaha wa INF na kufanyia majaribio kombora jipya inahatarisha usalama wa dunia nzima

 

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa na nchi zote duniani kuchukua hatua zinazofaa za kukabiliana na vitendo hivyo vya Marekani vya kuhatarisha usalama wa dunia na kujitoa kiholela katika makubaliano ya kimataifa. 

Jumapili iliyopita, Marekani ilifanyia majaribio kombora lake la masafa ya kati katika kisiwa cha San Nicolas, huko California. 

Hatua hiyo ya Marekani imechukuliwa baada ya serikali ya Donald Trump kujitoa katika mkataba wa kupambana na makombora ya nyuklia ya masafa ya wastani kwa kifupi, INF.

Tarehe pili mwezi huu wa Agosti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alitangaza rasmi kujitoa nchi yake katika mkataba wa INF.