Pompeo aendelea kutishia: Tutaendeleza mashinikizo dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i55663-pompeo_aendelea_kutishia_tutaendeleza_mashinikizo_dhidi_ya_iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa mara nyingine tena amesema kuwa mashinikizo dhdi ya Iran yataendelea hadi hapo nchi hii itakapobadili mwelekeo wake.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Aug 29, 2019 03:12 UTC
  • Pompeo aendelea kutishia: Tutaendeleza mashinikizo dhidi ya Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwa mara nyingine tena amesema kuwa mashinikizo dhdi ya Iran yataendelea hadi hapo nchi hii itakapobadili mwelekeo wake.

Baada ya Wizara ya Fedha ya Marekani kuiwekea Iran vikwazo vipya, Mike Pompeo aliandika jana katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Leo tumeziwekea vikwazo taasisi zinazojihusika na kusafirisha vifaa vya elektroniki na aloi nyeti za alumini vyenye thamani ya zaidi ya dola milioni moja. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ameongeza kuwa, nchi yake itaendelea kuishinikiza Iran hadi itakapobadili mwelekeo wake.

Katika kuendeleza uhasama wake dhidi ya Iran; Wizara ya Fedha ya Marekani jana Jumatano iliwawekea vikwazo shakhisia watano na mashirika matano kwa kisingizio cha kujihusisha na miradi ya makombora ya Iran. Serikali ya Marekani miezi kadhaa iliyopita iliiwekea Iran aina mbalimbali za mashinikizo na vikwazo hata hivyo imeshindwa kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya matakwa yake haramu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote inaeleza wazi kwamba itaendeleza miradi yake ya kiulinzi  kwa ajili ya kudhamini usalama wake kwa mujibu wa sheria na kanuni za kimataifa na bila ya kuzingatia upinzani wa madola ya kibeberu. 

Aidha akizungumza jana katika Tamasha la 15 la Shahidi Rajai hapa Tehran, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema wananchi wa Iran watashinda vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa umoja wao na muqawama.

Rais Hassan Rouhani akihutubia Tamasha la 15 la Shahidi Rajai

Alisema, maadui na wanaoitakia mabaya Iran daima wamekuwa na dhamira ya kulidhuru taifa hili; na akasisitiza kwamba, vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na maadui vitamalizika taifa la Iran likiwa ndio mshindi.