Sep 28, 2019 11:11 UTC
  • Iran yakosoa ukatili wa Marekani wa kumzuia Zarif kumtembelea balozi hospitalini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa amekosoa vikali kitendo cha kikatili cha Marekani cha kumzuia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kumtembelea Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ambaye amelazwa hospitalini mjini New York.

Sayyid Abbas Araqchi amesema katika ujumbe kuwa, "ni fedheha, jambo la kusikitisha na ukatili wa kupindukia kwa utawala wa Marekani kuuteka nyara ubinadamu kwa maslahi ya kisiasa."

Utawala wa Washington umetoa sharti la kichekesho la kumruhusu Dakta Zarif amtembelee hospitalini Majid Takht Ravanchi anayeugua ugonjwa wa saratani.

Marekani imeitaka Iran imuachie huru mfungwa mmoja wa Kimarekani, mkabala wa kumruhusu Zarif amtembelee mwanadiplomasia huyo hospitalini mjini New York.

Dakta Zarif na Majid Takh Ravanchi katika kikao cha huko nyuma

Serikali ya Marekani imechukua hatua inayokinzana na taratibu za kidiplomasia kwa kumwekea mpaka na kizuizi cha kutembea Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika mji wa New York.

Julai 31, Marekani ilitangaza kumwekea vikwazo na vizingiti vya kutembea Dakta Zarif, ambaye yuko mjini New York kushiriki kikao cha kila mwaka cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin alimtaja Zarif kama msemaji mkuu wa Iran duniani. Zarif alijibu kauli hiyo kwa kusema, "yaani, ukweli unauma kiasi hiki?"

Tags