Bloomberg: Vikwazo vya Marekani vimefali, uchumi wa Iran unaimarika
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56874-bloomberg_vikwazo_vya_marekani_vimefali_uchumi_wa_iran_unaimarika
Jarida la kimataifa la biashara la Bloomberg limethibitisha kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimefeli na kwamba uchumi wa nchi hii karibuni utaanza kuimarika.
(last modified 2026-03-21T11:32:05+00:00 )
Oct 27, 2019 02:39 UTC
  • Bloomberg: Vikwazo vya Marekani vimefali, uchumi wa Iran unaimarika

Jarida la kimataifa la biashara la Bloomberg limethibitisha kuwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimefeli na kwamba uchumi wa nchi hii karibuni utaanza kuimarika.

Jarida hilo limeandika kuwa 'mashinikizo ya juu kabisa' ya Marekani dhidi ya Iran yamefeli na sasa uthabiti unarejea katika bei za bidhaa, biashara, uzalishaji na sarafu ya riali ya Iran.

Ripoti hiyo ya Bloomberg imebaini kuwa moja ya dalili za kunza kuboreka uchumi wa Iran ni kuimarika riali kwa asilimia 40 mkabala wa dola ya Marekani tokea mwezi Mei. Benki Kuu ya Iran inatumia teknolojia mpya kudhibiti na kusimamia uuzaji na ununuzi wa fedha za kigeni na hivyo kuvuruga mitandao ya madalali waliokuwa wakiharibu soko.

Gavana wa Benki Kuu ya Iran Abdolnasser Hemmati amesema mfumuko wa bei umepungua na hali hiyo itaendelea hivyo katika miezi ijayo.

Riali ya Iran inazidi kuimarika

Aidha kutokana na kuimarika sekta ya uzalishaji katika viwanda vya Iran, Soko la Hisa la Tehran limetajwa kuwa soko bora zaidi duniani katika mwaka uliopita. Hali kadhalika uuzaji nje wa bidhaa zisizo za mafuta unatazamiwa kuvunja rekodi na kufika dola bilioni 40 mwaka huu.

Inatazamiwa kuwa mwaka huu, utakuwa wa kwanza katika historia ya kisasa ya Iran kwa bidhaa zisizo za mafuta kuwa na pato zaidi ya mafuta ambayo yanatazamiwa kuiletea nchi pato la dola bilioni 10 tu kufuatia vikwazo vya Marekani katika setka hiyo.

Makala hiyo ya Bloomberg imedokeza kuwa, ingawa vikwazo vya uuzaji mafuta ya Iran katika soko la kimataifa ni jambo ambalo limepelekea serikali ya Iran kupungukiwa na pato la fedha za kigeni lakini hivi sasa serikali inapanga bajeti yake pasina kutegemea pato la mafuta.

Ripoti hiyo ya Bloomberg imesema kimsingi uchumi wa Iran hautegemei mafuta kwani ni takribani asilimia 20 tu ya Pato Ghafi la Kitaifa  (GDP) la Iran ndilo hutegemea sekta ya mafuta.