Wairani waandamana nchi nzima kulaani ghasia za hivi karibuni
Raia wa Iran wamefanya maandamano makubwa baada ya swala ya Ijumaa kwa kupiga nara za 'Mauti kwa Marekani', 'Mauti kwa Israel' na 'Mauti kwa wafanya vurugu' ambapo pia sambamba na kutangaza kujitenga mbali na wafanya ghasia na kuchukia vitendo viovu vya kuibua machafuko nchini, wametangaza kuunga mkono usalama na amani nchini.
Itakumbukwa kuwa baada ya kufanyika marekebisho kuhusu bei ya mafuta nchini Iran siku ya Ijumaa iliyopita, wanainchi wa Iran walifanya maandamano ya amani mjini Tehran na baadhi ya miji mingine ya nchi hii. Hata hivyo kundi fulani la wafanya ghasia na majangili ambalo lilipata mafunzo kutoka nchi za maadui wa Iran lilijipenyeza kwenye maandamano hayo na kuanza kuharibu mali za umma na za watu binafsi, kuchoma mabenki, taasisi na kuharibuu magari ya wagonjwa na mabasi ya usafiri. Kufuatia vitendo hivyo wakazi wa mji wa Tehran leo wameshiriki katika maandamano makubwa ya baada ya swala ya Ijumaa kulaani wafanya ghasia na uharibifu sambamba na kuunga mkono usalama wa taifa hili. Mbali na hayo wakazi wa Tehran wametangaza pia kufanya maandamano makubwa siku ya Jumatatu kuwalaani wahuni na wafanya vurugu hao.
Aidha wakazi wa mji wa Mash'had nao wameshiriki katika maandamano kama hayo ambapo wameitangazia dunia uungaji mkono wao kwa maelekezo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kulinda usalama na amani ya nchi hii. Aidha wakazi wa mikoa ya Kohgiluyeh na Boyer-Ahmad, Khuzestan, Isfahan, miji ya Damghan, Mahdi Shahr, Sorkheh ya Semnan, mkoa wa Azerbaijan Mashariki na Magharibi, Gilan, Qum, Zanjan, Lorestan, Golestan, Sistan na Baluchestan nao kadhalika wamefanya maandamano makubwa ya kutangaza uungaji mkono wao kwa serikali na kulaani ghasia za hivi karibuni nchini hapa. Hii ni katika hali ambayo mahatibu wa swala za Ijumaa katika mikoa mbalimbali ya Iran pia sambamba na kusisitiza kuwa maandamano ya amani ni haki ya wananchi na kwamba ni wadhifa wa viongozi kutekeleza mahitaji yao, wamewataka pia viongozi wa serikali kusimamia vyema bei za sokoni ili kuwazuia baadhi ya watu wanaotafuta fursa ya kuibua ghasia nchini kutumia vibaya hali hiyo. Maandamano ya kulaani wazua ghasia na wafanya vurugu nchini Iran yalianza siku mbili zilizopita katika mikoa mbalimbali ya nchi hii ambapo washiriki wa maandamano hayo wametangaza kuiunga mkono serikali na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.