Zarif azilaumu nchi za Ulaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kibinadamu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezilaumu nchi za Ulaya kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kibinadamu na kuongeza kuwa, ni jukumu la nchi za Ulaya kutekeleza wajibu wa kuhusu watoto wadogo wa Iran wanaokwama kwenye matibabu kutokana na ugaidi wa kiuchumi unaofanywa na Marekani dhidi ya wananchi wa taifa hili.
Dk Mohammad Javad Zarif alisema hayo jana kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kusisitiza kuwa, lengo la ugaidi wa kiuchumi wa Marekani ni kuwatia matatizoni wananchi wa kawaida wa Iran. Aidha ameandika: Ugaidi wa kiuchumi wa Marekani unasababisha watu kupoteza maisha yao nchini Iran.
Vile vile amesema, nchi tatu kubwa za Ulaya na Umoja wa Ulaya wenyewe unapaswa uache kiburi cha kutoa vitisho na ahadi hewa, na badala yake zitekeleze kutekeleza majukumu yao ya kibinadamu, na kwamba mashirika ya madawa barani Ulaya nayo yana wajibu wa kutimiza ahadi na majukumu yao ya kibinadamu ya kuwapelekea madawa watoto wa Kiirani wanaosumbuliwa na maradhi ya EB, na sio kukaa na kutoa ahadi hewa na vitisho vya kiburi.
EB ni kifupi ugonjwa wa "Epidermolysis bullosa" ambayo ni maradhi ya kurithi ya ngozi na ni hatari sana kwa watoto kwani mtu anayekumbwa na ugonjwa huo huwa kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa wa kensa.
Mwezi Mei 2018, rais wa Marekani, Donald Trump alijitoa kivyake na bila ya sababu katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele katika kuyafanikisha. Baada ya kujitoa kwenye mapatano hayo yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1, Marekani iliirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa makubaliano hayo.