Tehran yatoa onyo kali kwa maadui: Msivuke mistari myekundu ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57675-tehran_yatoa_onyo_kali_kwa_maadui_msivuke_mistari_myekundu_ya_iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametoa onyo kali kwa maadui akiwaambia wasivuke mistari myekundu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 04, 2019 08:36 UTC
  • Tehran yatoa onyo kali kwa maadui: Msivuke mistari myekundu ya Iran

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH ametoa onyo kali kwa maadui akiwaambia wasivuke mistari myekundu ya Iran.

Meja Jenerali Hossein Salami ametoa onyo hilo leo Jumatano katika Kongamano la Mashahidi 92 elfu wa Jeshi la Basiji hapa Tehran na kusisitiza kuwa, iwapo adui atafanya chokochoko zozote zile, basi taifa la Iran litamuangamiza huko huko aliko.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH vile vile amezungumzia mwamko na muono wa mbali wa wananchi wa Iran katika matukio ya hivi karibuni humu nchini na kusisitiza kuwa, wiki zilizopita, wananchi wa Iran walitoa pigo jingine kubwa kwa mabeberu hususan Marekani.

Jeshi la kujitolea la wananchi wa Iran (Basiji)

 

Amesema, katika fitna za hivi karibuni za maadui wa taifa la Iran, madola ya kiistikbari yalitaka kutumia fitna hizo kufidia vipigo vya mara kwa mara yanavyopata kutoka kwa taifa la Iran lakini wameshindwa.

Ameongeza kwa kusema: Maadui walitaka kuunganisha fitna hiyo na mashinikizo yao ya kiwango cha juu zaidi dhidi ya Iran lakini wananchi wa taifa hili la Kiislamu walikuwa macho na kufelisha kikamilifu njama zao hizo.

Meja Jenerali Salami aidha amesema, taifa la Iran limeweza kusimama imara katika kulinda matukufu yake ya kitaifa na Kiislamu kwa zaidi ya miaka 40 sasa na kuongeza kuwa, Iran inaendelea mbele na njia yake kwa nguvu na umakini wa hali ya juu na karibuni hivi itakuwa dola kubwa duniani.