Waziri wa Mafuta wa Iran: Hatutafumbia macho haki ya Iran
Waziri wa Mafuta wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kamwe Tehran haitofumbia macho haki yake ya msingi.
Bijan Zangeneh ambaye aliyasema hayo kabla ya kuanza mkutano wa 177 wa wakuu wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ameongeza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitokubali kupunguza kwa namna isiyo ya kimantiki uzalishaji wake wa mafuta hata kwa pipa moja. Amesisitiza kwamba, hadi sasa uzalishaji mafuta wa Iran umetoka katika soko la kimataifa na kwamba wale wanaozalisha zaidi nishati hiyo ndio wanaopaswa kupunguza uzalishaji wao.
Bijan Zangeneh ameongeza kwamba kutokana na mazingira maalumu, Iran imepunguza bila ya hiari yake uzalishaji wake, kama ambavyo inazalisha kwa kiwango cha chini kihistoria, na kwa mantiki hiyo wale ambao wanazalisha zaidi mafuta ndio wanaotakiwa kupunguza uzalishaji wao. Mkutano wa 177 wa wakuu wa Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ulianza jana Alkhamisi mjini Vienna, Austria. Mawaziri wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo wanajadili namna ya kulinda mlingano wa bei ya mafuta sokoni, kuendelea na hali ya sasa au kupunguza mapipa laki nne katika uzalishaji wao. Makubaliano ya kupunguza kiwango cha mapipa milioni moja na laki mbili kwa siku yatafikia tamati mwishoni mwa mwezi Machi mwakani.