UN: Hakuna ushahidi kwamba Iran ilihusika na mashambulizi dhidi ya Aramco, Saudia
Ripoti iliyotolewa na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa Saudi Arabia imesema kuwa, hawajapata ushahidi wa aina yoyote unaothibitisha kuwa Iran ilihusika na mashambulizi dhidi ya taasisi za mafuta za Saudi Arabia.
Ripoti hiyo ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa, haiwezekani kuthibitisha madai ya Washington na Riyadh kwamba Iran ilihusika na mashambulizi dhidi ya taasisi za mafuta za Saudia. Mtandao wa habari wa Bloomberg umetangaza kuwa, katika ripoti yake ya kila baada ya miezi sita, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa umoja huo hauwezi kuthibitisha kwamba, makombora na ndege zisizo na rubani zilizotumiwa kushambulia taasisi za mafuta za Saudi Arabia zilitokea Iran.
Itakumbukwa kuwa tarehe 14 Septemba mwaka huu 2019, Kikosi cha Ndege Zisizo na Rubani cha Jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi kilishambulia vituo vikubwa vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais mashariki mwa Saudia ambavyo vinamilikiwa na shirika la Aramco. Mashambulizi hayo yaliyofanyika kwa kutumia ndege 10 zisizo na rubani yalisimamisha nusu ya uzalisha wa mafuta wa Saudia. Mashambulizi hayo yalifanywa kulipiza kisasi cha mauaji na jinai zinazofanywa na Saudia Arabia na washirika wake dhidi ya taifa la Yemen
Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakitoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran na kudai kuwa Tehran ilihusika katika oparesheni hiyo ya Wayemen. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali kuhusika na mashambulizi hayo na imetaja madai dhidi yake kuwa yasiyo na msingi.