Usalama, mhimili wa hotuba ya Zarif katika Mkutano wa Doha
-
Muhammad Javad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, baadhi ya nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi zinatumia ukosefu wa mlingano wa nguvu uliopo katika eneo hilo kama fursa ya kulidhibiti eneo hilo, na kwamba mzingiro wa Saudi Arabia dhidi ya Qatar na vita vya nchi hiyo huko Yemen ni mifano hai ya makosa hayo ya kimahesabu yenye maafa makubwa.
Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo katika Mkutano wa Doha ambako pia alibainisha mtazamo wa Iran kuhusiana na amani na usalama wa Ghuba ya Uajemi. Zarif amesema kuwa: "Ukosefu wa mlingano wa nguvu baina ya nchi za Ghuba ya Uajemi umezusha mgogoro katika eneo hili."
Katika mazungumzo yake na Ban Ki-moon Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefafanua mpango wa Iran kwa ajili ya amani ya Hormuz. Awali Zarif pia alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi za Oman na Kuwait na kufanya nao mashauriano kuhusu kadhia hiyo.
Matamshi na mashauriano haya ya Zarif yana nukta mbili muhimu:
Kwanza ni kwamba, katika mazungumzo hayo kumetolewa taswira ya wazi ya stratijia ya Iran kwa ajili ya kulinda amani ya Ghuba ya Uajemi ambayo inaakisi mtazamo wa Tehran kuhusu usalama wa eneo hilo.
Pili ni kwamba, mashauriano hayo yanaonesha siasa za nje za Iran kuhusiana na eneo hilo ambazo msingi wake ni kujenga hali ya kuaminiana baina ya nchi zote za kanda hii. Ni kwa msingi huo ndipo Jamhuri ya Kiislamu ikatoa pendekezo la kutiwa saini mkataba wa kutoshambuliana baina ya nchi za kanda hii na kushirikishwa nchi hizo zote katika kulinda amani. Itakumbukwa kwamba katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu alitangaza mpango wa Tehran wa amani ya Hormuz, Hormuz Peace Endeavor (HOPE). Mpango huo wenye faida kwa nchi zote za Ghuba ya Uajemi unajumuisha njia za pamoja za kulinda amani katika eneo hilo kwa kutegemea uwezo wa nchi za kanda hiyo na si madola ya kigeni. Suala hilo ambalo limesisitizwa pia katika mazungumzo na mashauriano ya Zarif huko Doha, linaonekana kwenda kinyume na harakati za Marekani katika eneo hilo.
Mhadhiri na mchambuzi wa siasa wa Marekani, Denis Atler anaashiria lengo la jitihada za Marekani za kutaka kuunda muungano wa baharini katika Ghuba ya Uajemi na kusema: "Marekani inataka kulitwisha eneo la Ghuba ya Uajemi kikosi chake kitakachoundwa na askari wake na washirika wake wa Ulaya." Mchambuzi huyo wa masuala ya siasa anaongeza kuwa: "Mpango wowote wa amani na kulinda usalama katika Ghuba ya Uajemi unapaswa kupasishwa na nchi zote za eneo hilo ikiwemo Iran na kusimamiwa na Umoja wa Mataifa."
Inatupasa kusema hapa kuwa, miongoni mwa sababu kuu zinazozuia kuwepo ushirikiano wa nchi za Ghuba ya Uajemi katika masuala ya usalama ni maslahi haramu ya madola makubwa ya kibeberu ambayo yanazusha migogoro na hali ya ukosefu wa amani kwa shabaha ya kupata fursa ya kuuza silaha na kudhibiti raslimali na utajiri wa eneo hilo.
Kuhusiana na suala hilo Dakta Javad Zarif amesema katika Mkutano wa Doha kwamba: "Katika kipindi cha baina ya mwaka 2014 na 2018 nchi za Ghuba ya Uajemi zilinunua karibu ya robo ya silaha zote zilizotengenezwa duniani na kiwango kikubwa cha silaha hizo haribufu kimeuzwa na Marekani."
Pamoja na hayo yote Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa umuhimu mkubw suala la kulinda usalama wake na kujiepusha na vitisho na katika suala hilo sio tegemezi kwa upande wowote. Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami anasema: "Taifa la Iran linapaswa kuwa imara na tayari wakati wote katika nyuga tofauti ili liendelee kulinda nguvu zake za kumzuia adui hata asifikirie kulivamia kijeshi taifa hili la Kiislamu."
Suala ambalo liko wazi ni kwamba vita, vikwazo na kuunda miungano bandia katika eneo la Ghuba ya Uajemi haviwezi kulipigisha magoti taifa la Iran au kuathiri mantiki yake ya kuchumua maamuzi muhimu. Kwa msingi huo mbali na kutilia mkazo suala la kuwepo ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi za Ghuba ya Uajemi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza pia udharura wa kuwa na nguvu kwa ajili ya kukabiliana na vitisho.